Author: Honest Mwanitega

YOUNG AFRICANS YAREJEA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Young Africans imeendelea kuonyesha kwanini inaiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika baada ya kushinda 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kukwea hadi nafasi ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Young Africans iliyokuwa ya kwanza kuruhusu bao dakika nne kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kupitia kwa Edgar William haikukata tamaa na zikisalia dakika tatu mchezo kwenda mapumziko ilisawazisha kupitia kwa Laurindo Dilson akitumia mkwaju wa penati baada ya Andy Bikoko kumchezea rafu mchezaji wa Young Africans.

Kipindi cha pili Laurindo aliongeza bao na Prince Dube kupigilia msumari wa tatu na kupeleka furaha kwa ‘Wananchi’ na huzuni kwa ‘wakulima wa zabibu’.

Laurindo Dilson ‘Depu’ amekuwa na kiwango bora kwenye Ligi Kuu ya NBC tangu ajiunge na Young Africans akifunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao moja huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na kufanikiwa kuifanya Young Africans kurejea kileleni ikifikisha jumla ya alama 22.

Young Africans inaungana na Azam Fc na kuwa timu pekee ambazo hazijapoteza mchezo hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC na zikiwa zimeruhusu mabao machache pia (2) huku ‘Wananchi’ wakiongoza kwa kufunga mabao hadi sasa (21).

Mkoani Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani Coastal Union ililazimishwa sare ya bao moja na timu ya KMC ikiwa sare ya pili kwa KMC iliyopoteza michezo nane hadi sasa na ikishika nafasi ya mwisho ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

KMC iliyoshinda mchezo mmoja pekee hadi sasa imefanikiwa kufikisha mabao matatu kwenye ligi hiyo ikiwa timu iliyofunga mabao machache hadi sasa huku ikiongoza kwa kufungwa mabao mengi (18).

Sare hiyo inaifanya Coastal Union iliyopoteza mchezo wao uliopita ugenini dhidi ya Namungo kukwea hadi nafasi ya 11 ikifikisha jumla ya alama 10 ikiwa imepata ushindi kwenye michezo miwili pekee.

 

SIMBA YABANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Simba imeshindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na timu ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

‘Mnyama’ alikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Ellie Mpanzu mapema kipindi cha kwanza kabla ya Mtibwa kusawazisha kupitia kwa Magata Fredrick bao lililowapa Mtibwa alama moja muhimu ugenini dhidi ya timu inayowakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imeshindwa kupata ushindi nyumbani kwa mara pili mfululizo baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam kwa mabao 2-0.

Sare hiyo inaifanya Simba kukaa nafasi ya nne ikifikisha alama 13 huku Mtibwa ikifikisha alama 11 na kusalia nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo Januari 19 kwa mchezo mmoja kati ya Young Africans itakayokuwa mwenyeji wa Mashujaa kwenye uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Endapo Young Africans itafanikiwa kupata ushindi leo itaishusha timu ya JKT Tanzania na kukwea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC.

AZAM YA IBENGE NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Azam yenye maskani yake kwenye uwanja wa Azam Complex imekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu ikiwa haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC hadi sasa.

Mchezo uliopita Azam ilishinda dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa nyumbani kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Yahya Zayd, Feisal Salum na Jephte Kitambala huku mabao yote yakifungwa kipindi cha kwanza na kudumu kwa dakika zote 90.

Azam imefunga mabao 9 na kuruhusu mabao mawili pekee huku ikiwa imetoka sare michezo mitatu hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Timu hiyo inaingia mawindoni kulisaka taji la Ligi Kuu ya NBC baada ya kulikosa kwa miaka 13 wakiwa na matumaini ya kufanya hivyo msimu huu chini ya kocha Florent Ibenge ambaye hadi sasa amewasaidia kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza kuanzia timu hiyo ianzishwe.

Mara ya mwisho timu ya Azam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ilikuwa mwaka 2013 na walitwaa bila kupoteza mchezo wowote.

NBC CHAMPIONSHIP YAFIKA PATAMU.

IKIKAMILISHA mizunguko 15 Ligi ya NBC Championship imepamba moto timu zote zikiwa zimecheza michezo 15 huku zikisaliwa na michezo 15 kufunga msimu.

Geita Gold inaongoza mbio za ubingwa ikiwa na alama 37 baada ya kushinda michezo 11 huku ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa.

Kagera Sugar inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 36 ikipoteza mchezo mmoja pekee kwenye mzunguko wa 15 dhidi ya ‘wababe’ wa mkoa wa Tabora timu ya Mbeya Kwanza inayokamata nafasi ya tatu ikiwa na alama 34.

Transit Camp inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 33 ikizidiwa alama nne pekee na vinara wa ligi hiyo timu ya Geita Gold, Transit ikiwa imeshinda michezo 10 hadi sasa, ikipoteza miwili na kutoa sare mitatu.

Bingwa wa ligi ya Championship ya NBC atapata Kikombe na kupanda daraja moja kwa moja hadi Ligi Kuu ya NBC, mshindi wa pili akipanda daraja huku mshindi wa tatu na wa nne wakicheza mchezo wa mtoano na timu itakayoshinda kwenye matokeo ya jumla itacheza na timu ya Ligi Kuu ya NBC ili kupata timu moja itakayoshiriki ligi hiyo ya nne kwa ubora Afrika msimu wa 2026/27.

AZAM, COASTAL WANA KIKAO LIGI KUU YA NBC LEO.

MATAJIRI wa Chamazi timu ya Azam leo itakuwa na kibarua cha kusaka alama tatu muhimu nyumbani dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuanza mwaka 2026 vibaya baada ya kupoteza kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Young Africans Azam itavaana na Coastal inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Azam inayoshika nafasi ya tisa bado haijapoteza mchezo wowote wa ligi hiyo msimu huu sawa na timu ya Young Africans ambayo pia haijapoteza mchezo.

Tayari Coastal Union imepoteza michezo mitatu msimu huu ikishinda miwili na kutoa sare mitatu ikiwa imekusanya jumla ya alama tisa hadi sasa.

Huu ni mchezo pekee wa Ligi Kuu ya NBC unaopigwa leo baada ya jana timu ya Dodoma Jiji kulazimishwa sare ya bao moja nyumbani na Singida Black Stars.