KILELE cha ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25 kinatarajiwa kufikiwa leo kwa mchezo wa kukabidhi ubingwa kati ya Mtibwa Sugar na Mbeya City utakaopigwa leo kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam saa 2:00 usiku.
Ligi hiyo ilifika tamati Mei 11, kwa michezo nane kupigwa na Mtibwa Sugar kumaliza bingwa na kupanda daraja akifikisha jumla ya alama 71 huku Mbeya City ikimaliza nafasi ya pili na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 sambamba na Mtibwa.
Mtibwa Sugar imerejea Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni msimu mmoja pekee tangu kushuka daraja huku Mbeya City ikitumia misimu miwili kurejea ligi hiyo.
Mchezo wa leo utarushwa mubashara TV3 na utakuwa sambamba na sherehe za kukabidhi ubingwa kwa timu ya Mtibwa Sugar baada ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ya Championship ya NBC.