Author: Honest Mwanitega

MASHUJAA, YOUNG AFRICANS, NAMUNGO, VITANI LEO LIGI KUU YA NBC.

VIWANJA vitatu vya Ligi Kuu NBC vinaendelea kutoa burudani leo kwa ratiba ya michezo mitatu inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikihitaji alama kwa malengo tofauti msimu huu.

Macho mengi yataelekezwa katika viwanja vya Lake Tanganyika, Kigoma, KMC Complex, Dar es Salaam na Majaliwa, Lindi ambako mapambano ya kibingwa yanayohusisha vita ya nafasi za juu pamoja na presha ya kushuka daraja kupamba moto.

Katika mchezo wa mapema utakaochezwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Mashujaa FC watawakaribisha Pamba Jiji kwenye mechi inayobeba uzito mkubwa kwa timu zote mbili.

Mashujaa wakiwa nyumbani watataka kutumia faida ya mashabiki wao kutafuta ushindi muhimu baada ya kushindwa kupata matokeo mchezo uliopita dhidi ya Fountain Gate huku Pamba Jiji wakisaka matokeo chanya yatakayowaweka kwenye nafasi salama zaidi kwenye msimamo wa ligi.

Mechi hii inatarajiwa kuwa ya nguvu nyingi katikati ya uwanja kutokana na timu zote kupenda kucheza kwa presha huku wakitumia zaidi viungo wa kati kuliko viungo wa pembeni.

Mchezo mwingine mkubwa wa leo utakuwa kati ya Young Africans watakapowakaribisha Tanzania Prisons katika uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam saa 12:30 jioni.

Young Africans wakiwa kwenye mbio za kuwania ubingwa hawana nafasi ya kupoteza alama na ushindi wa leo unaweza kuongeza presha kwa wapinzani wao kwenye kilele cha msimamo.

Tanzania Prisons nao wanakuja na morali ya kutafuta matokeo ya kushtua wakifahamu kupata alama dhidi ya timu kubwa kunaweza kubadili kabisa mwenendo wao wa msimu huu.

Usiku wa leo saa 3:00 usiku timu ya Namungo FC itawakaribisha JKT Tanzania kwenye uwanja wa Majaliwa katika pambano jingine linalosubiriwa kwa hamu.l kukamilisha burudani za siku ya leo.

Namungo wamekuwa timu ngumu sana inapocheza nyumbani jambo linalowapa nguvu dhidi ya JKT Tanzania ambao nao mara nyingi huonekana kuwa na nidhamu kubwa ya kiuchezaji chini ya kocha Ahmad Ally ambaye pia ni kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Hii inaweza kuwa moja ya mechi ngumu zaidi ya leo kutokana na ubora unaokaribiana kwa pande zote mbili.

Kwa ujumla, ratiba ya leo inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye msimamo wa ligi hasa kwa timu zinazowania ubingwa, nafasi za juu na zile zinazokwepa hatari ya kushuka daraja.

Mashabiki wanatarajia kuona mabao, ushindani mkali na matokeo yatakayoongeza joto la NBC Premier League kuelekea hatua za mwisho za msimu huku kila timu ikitaka kumaliza kwa furaha na mafanikio.

DODOMA JIJI, MBEYA CITY ZAWASHA MOTO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu NBC imeendelea jana kwa michezo miwili iliyotoa burudani ya viwango ambapo Dodoma Jiji iliichapa Fountain Gate mabao 3-0, huku Mbeya City ikiibuka na ushindi wa kusisimua wa 3-2 dhidi ya KMC.

Katika mchezo uliopigwa Airtel Stadium, Singida, wenyeji Dodoma Jiji walionyesha ubora mkubwa hasa kipindi cha pili na kuondoka na alama tatu muhimu mbele ya Fountain Gate baada ya kipindi cha kwanza kumalizika wakiwa kifua mbele kwa bao moja kupitia kwa nahodha Augustino Nsata aliyefunga dakika ya 38.

Iddi Kipagwile aliongeza bao la pili dakika ya 69 na dakika za nyongeza Yasin Mgaza alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu dakika ya 90+1 na kuifanya Dodoma kushinda kwa kishindo 3-0.

Ushindi huo unaifanya Dodoma kuendelea kuimarisha nafasi yao katikati ya msimamo wa ligi ikikaa nafasi saba ikiwa imekusanya alama 24.

Kwa upande mwingine, katika mchezo uliochezwa Tanzanite Kwaraa, Manyara, mashabiki walishuhudia moja ya mechi tamu zaidi za wiki hii baada ya Mbeya City kuifunga KMC 3-2.

KMC ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Oscar Paul dakika ya 44, na kwenda mapumziko wakiwa mbele.

Kipindi cha pili Mbeya City walibadilika kabisa, wakisawazisha kupitia Riphat Msuya dakika ya 64, kabla ya Adili Buha kufunga kwa penalti dakika ya 76 na kuwapa uongozi wenyeji.

Hata hivyo, KMC hawakukata tamaa na walifanikiwa kusawazisha dakika ya 78 kupitia Juma Shemvuni, jambo lililoongeza presha kubwa kwa wenyeji Mbeya City.

Wakati mchezo ukionekana kuelekea sare, Said Naushad alitokea kuwa shujaa wa Mbeya City kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 86, na kuamsha shangwe kubwa Tanzanite Kwaraa. 

Matokeo hayo yana maana kubwa kwenye mbio za msimamo wa ligi, hasa kwa Mbeya City ambao walikuwa wanahitaji sana ushindi huo kujinasua kutoka maeneo ya hatari ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kwa ujumla, jana ilikuwa siku ya mabao 8 kwenye michezo miwili, ushindi wa kishindo kwa Dodoma Jiji na ushindi wa jasho kwa Mbeya City, matokeo ambayo yanaongeza ushindani mkubwa zaidi msimu huu.

FIRST LEAGUE YA MOTO! BANDARI, RHINO ‘VINARA’ MBIO ZA KUPANDA NBC CHAMPIONSHIP.

MSIMU wa First League 2025/26 umeendelea kutoa ushindani mkubwa baada ya kila timu kucheza mechi tisa huku vita ya kusaka nafasi ya kupanda Ligi ya NBC Championship ikizidi kupamba moto katika makundi yote mawili.

Kwenye kundi A timu ya Bandari Tanzania inaonekana kuwa na kasi kubwa zaidi baada ya kujikusanyia alama 20, wakiongoza msimamo mbele ya Nyumbu yenye alama 18 huku tofauti ya alama mbili pekee kati ya timu hizo ikionyesha wazi kuwa mbio za kileleni bado hazijaamuliwa na kila mchezo uliosalia utakuwa na uzito mkubwa.

Takwimu za Bandari zinaonyesha uimara mkubwa, wakiwa na ushindi kwenye michezo sita, sare mbili na kupoteza mchezo mmoja pekee, huku safu yao ya ushambuliaji ikiwa tayari imefunga mabao 17. 

Nafasi ya tatu inashikiliwa na Cosmopolitan ambayo haipo mbali baada ya kufikisha alama 16, jambo linalofanya kundi A kuwa moja ya makundi yenye ushindani mkali zaidi ambapo tofauti ndogo ya alama kati ya timu tatu za juu ikiashiria kuwa mzunguko wa pili unaweza kubadili kabisa ramani ya msimamo.

Kwa upande wa kundi B timu ya Rhino Rangers imekuwa bora zaidi hadi sasa ikiwa na alama 24 baada ya mechi 9 ikionyesha ubora mkubwa kwa kushinda michezo minane na kupoteza mmoja pekee.

Safu ya ushambuliaji ya ‘maafande’ hao imefunga jumla ya mabao 21, idadi kubwa zaidi kwenye makundi yote mawili ya First League huku wakiruhusu mabao saba pekee huku hii ikiwa sababu kubwa ya kuwa kwenye nafasi kubwa ya kumaliza kileleni na kukata tiketi ya moja kwa moja kuelekea NBC Championship. 

Timu za IAA na Endument bado wapo kwenye mbio hizo wakishika nafasi ya pili na tatu ingawa wanalazimika kuongeza kasi ili kuzuia Rhino Rangers wasiweke uwiano mkubwa wa alama zaidi kileleni.

VITA YA MTOANO NA JANGA LA KUSHUKA DARAJA.

Mbali na vita vya juu, pambano la kujiokoa kushuka daraja pia limeanza kuchangamka sana.

Katika kundi A, Dar City inaonekana kuwa kwenye kipindi kigumu zaidi baada ya kubaki mkiani na alama 4 pekee, huku ikiwa tayari imeruhusu mabao 24 na kuwa na rekodi mbaya ya safu ya ulinzi ambayo imekuwa sababu kubwa ya timu hiyo kuwa katika hatari kubwa ya kushuka daraja.

Kwa kundi B hali ni mbaya zaidi kwa ‘Wanajeshi wa mpakani’ timu ya Biashara United ambayo hadi sasa ina deni la alama -1lililotokea baada ya kushindwa kufika uwanjani kwenye michezo miwili na kupokwa alama na mamlaka za soka kitu kinachoonyesha wazi namna walivyoanza msimu vibaya na jinsi kila mchezo uliosalia utakavyokuwa wa kama fainali kwao.

MICHEZO IJAYO KUAMUA HATMA.

Ratiba ya michezo ijayo inaweza kubadilisha kabisa sura ya misimamo yote miwili hasa kwa kundi A ambapo Bandari bado wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Nyumbu, Green Warriors na Cosmopolitan. 

Kwa kundi B macho yote yataelekezwa kwa Rhino Rangers kuona kama watakuwa na muendelezo mzuri au wapinzani wao wataanza kupunguza ‘pengo’ la alama.

Kwa ujumla, First League msimu huu imeonyesha ushindani wa hali ya juu, mabao mengi, na presha kubwa kuanzia nafasi za juu hadi chini ya msimamo na endapo kasi hii itaendelea mzunguko wa pili unaweza kuwa mmoja wa misimu yenye utofauti mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa.

AZAM YAONGEZA PRESHA KWENYE ‘KILELE’ CHA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Azam imeonyesha ubora na ukomavu mkubwa baada ya kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Airtel Stadium, Singida.

Baada ya kutoka sare mbili mfululizo bila kufungana, kikosi hicho cha kocha Florent Ibenge kilirejea kwa nguvu na kuonyesha dhamira ya kupambania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Bao la kwanza la Azam lilifungwa mapema kipindi cha pili kupitia kwa nahodha Lusajo Mwaikenda aliyemalizia kwa ustadi mpira wa krosi uliotengenezwa na Iddy Seleman ‘Nado’.

Dakika chache baadaye, staa wa timu hiyo Feisal Salum “Fei Toto” aliandika bao la pili kwa shuti la utulivu baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa ‘Nado’ bao ambalo liliongeza presha kubwa kwa wenyeji Singida.

Singida Black Stars walijitahidi kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao moja kupitia kwa Ayubu Lyanga dakika ya 71, lakini juhudi zao za kusawazisha ziligonga mwamba mbele ya safu imara ya ulinzi ya ‘Matajiri wa chamazi’.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kuendelea kuwepo kwenye mbio za ubingwa msimu huu ikikwea hadi nafasi ya pili baada ya kukusanya alama 32 huku ikionyesha kuwa bado ni tishio kubwa kwa vigogo wengine wa ligi, hasa kuelekea ‘duru’ la mwisho la Ligi Kuu ya NBC.

NBC CHAMPIONSHIP ‘YAFUKUTA’ MZUNGUKO WA 21.

Ligi ya NBC Championship imetimiza mzunguko wa 21 huku ushindani ukizidi kupamba moto, timu zikionyesha wazi dhamira ya kupigania kupanda daraja kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu ujao na nyingine zikipambana kusalia ligi hiyo msimu ujao.

Katika hatua hii ya ligi, kila alama imekuwa ya thamani kubwa, huku timu za juu ambazo ni Geita Gold, Kagera Sugar,Mbeya Kwanza na Transit Camp zikionekana kuongeza kasi ili kujihakikishia nafasi za moja kwa moja za kupanda daraja na mapambano hayo yameifanya ligi kuwa na mvuto mkubwa zaidi, ambapo matokeo ya kila wiki yamekuwa yakibadilisha mwelekeo wa msimamo wa ligi hiyo.

Kwa upande wa katikati ya msimamo penye timu za Bigman yenye alama yenye alama 27 ikishika nafasi ya saba, KenGold inafuata ikiwa na alama 26 sawa na Songea United na Gunners inayoshika nafasi ya 10 ikiwa imekusanya alama 23 hali inaendelea kuwa ngumu kwa timu hizo ambazo zinajikuta zikihitaji ushindi mfululizo ili kuepuka kuingia kwenye hatari ya kushuka daraja na jambo hil limeongeza ushindani mkali, kwani tofauti ya pointi kati ya timu hizo ni ndogo sana.

Wakati huo huo, timu za ‘mkiani’ ambazo ni African Sports inayoshika nafasi ya 15 na Barberian inayoshika nafasi ya 16 zinapambana kwa nguvu zote kujiokoa, hali inayofanya kila mechi kuwa ya ushindani wa hali ya juu na presha imekuwa kubwa kwa wachezaji na benchi la ufundi, huku makosa madogo yakigharimu matokeo makubwa.

Ligi hiyo pia imeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wachezaji kuonyesha viwango vyao, ambapo baadhi yao kama Obrey Chirwa anayekipiga kwenye timu ya Kagera Sugar anayeongoza mbio za ufungaji na Ramadhan Karanje wa B19 aliyeibuka mchezaji bora wa mwezi Februari wameanza kuvutia macho ya klabu kubwa kutokana na kiwango wanachoonyesha uwanjani.

Kadri msimu unavyozidi kusonga mbele, wachambuzi wa soka wanaamini kuwa ushindani utaongezeka zaidi, hasa katika nafasi za juu zinazoongozwa na kinara Geita Gold zinazotoa tiketi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC pamoja na zile za mkiani zinazohusisha mapambano ya kuepuka kushuka Ligi ya First League.

Kwa sasa, macho ya wadau wa soka yameelekezwa kwenye hatua zijazo za ligi hiyo iliyosimama kwa takribani mwezi mmoja, wakisubiri kuona ni timu zipi zitafanikiwa kuhimili presha na kuandika historia ya kupanda daraja mwishoni mwa msimu na zipi zitaweza kuamka na kusalia kwenye ligi msimu ujao.