Author: Honest Mwanitega

MANUNGU TISHIO KWA TIMU NGENI NBC CHAMPIONSHIP.

UWANJA wa Manungu uliopo Mkoani Morogoro umekuwa tishio kwa timu zinazoenda kucheza dhidi ya mwenyeji wa uwanja huo Mtibwa Sugar baada ya timu hiyo kushinda michezo 12 hadi sasa kwenye uwanja huo na kuwa idadi kubwa hadi sasa kwenye Ligi ya NBC Championship.

Mtibwa iliongeza idadi ya ushindi wikiendi iliyopita baada ya kutoka nyuma dhidi ya Biashara United iliyokuwa ikiongoza 2-0 kipindi cha kwanza na Mtibwa kumaliza mchezo kwa ushindi wa 3-2.

Uwanja wa Kambarage unaotumiwa na Stand United unashika nafasi ya pili baada ya timu mwenyeji wa uwanja huo Stand United kushinda michezo 11 hadi sasa huku idadi hiyo ikitimia baada ya Stand kushinda mchezo uliopita kwa mabao 3-0 dhidi ya African Sports ya Tanga.

Nyankumbu, Geita uwanja unaotumiwa na Geita Gold unafuata baada ya Geita kushinda michezo 11 idadi sawa na Stand inayotumia uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

STAND, GEITA, MBEYA CITY MOTO HAUZIMI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

LIGI ya Championship ya NBC imeendelea jana kwa michezo mitatu iliyoshuhudia mabao nane yakifungwa na magolikipa watatu wakimaliza michezo bila kuruhusu bao.

Stand United ilikuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga na kushuhudia Stand ikikusanya alama zote tatu baada ya ushindi wa bao moja lililofungwa na Omar Issa mapema dakika ya sita kwa mkwaju wa penati.

Matokeo hayo yanaifanya Stand kufikisha alama 49 na kukaa nafasi ya tatu huku ikiwa timu ya pili kwa kushinda michezo mingi msimu huu ikishinda 15 sawa na timu ya Geita Gold.

Geita Gold ilikuwa nyumbani kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita na kufanikiwa kuichapa Mbeya Kwanza mabao 3-0 yaliwekwa kambani na Andrew Simchimba (2) na Jackson Suluja aliyefunga moja.

Geita inafikisha alama 48 na kusalia nafasi ya nne nyuma ya Stand United inayoshika nafasi ya tatu na Mbeya City inayoshika nafasi ya pili na kufanya upinzani wa kucheza Ligi Kuu ya NBC msimu ujao kuzidi kushika kasi.

Mchezo wa mwisho ulikuwa kati Mbeya City iliyoshusha mvua ya mabao 4-0 dhidi ya timu ya Kiluvya kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya huku mchezaji wa Mbeya City Mwami Thobias akifunga mabao matatu na Adil Buha kufunga moja.

Ushindi huo umeifanya Mbeya City kusalia nafasi ya pili ikifikisha alama 49 huku ikiwa kinara wa mabao hadi sasa baada ya kufunga (45) huku Cosmopolitan ikiwa timu iliyofunga mabao machache (15).

HAUSUNG, RHINO VINARA MBIO ZA KUPANDA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

LIGI ya First League inazidi kupamba moto kwenye viwanja tofauti huku timu za Hausang ya Makambako Njombe na Rhino Rangers ya Tabora zikiongoza mbio hizo.

Timu ya Hausang inaongoza kundi A baada ya kucheza michezo 12 ikishinda michezo sita, sare nne na kupoteza miwili huku ikifanikiwa kukusanya alama 22.

Timu ya Magnet inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na alama 11 baada ya kushinda michezo miwili, kupoteza mitano na sare tano.

Rhino Rangers inashikilia usukani wa kundi B ikikusanya alama 28 baada ya kushinda michezo tisa, sare mchezo mmoja na kupoteza michezo miwili.

Rhino inaongoza pia kwenye kupachika mabao ikifunga (30) huku Ruvu Shooting ikiwa timu iliyofunga mabao machache hadi sasa ikifunga mawili pekee.

Kinara wa kundi A atakutana na kinara wa kundi B katika mchezo wa mwisho wa msimu ili kumpata bingwa wa Ligi ya First League msimu wa 2024/25.

SIMBA KUWAVAA DODOMA LEO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha timu za Simba dhidi ya Dodoma kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar.

Simba iliyoshinda mchezo wake wa Ligi Kuu ya NBC uliopita ugenini dhidi ya Coastal Union kwa mabao 3-0 inakutana na Dodoma Jiji iliyolazimishawa suluhu na Coastal kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Timu ya Simba inahitaji alama tatu leo ili kujiweka nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa NBC msimu huu huku Dodoma ikihitaji kupata ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Mchezo huu ni wa kiporo ulioahirishwa baada ya timu ya Dodoma Jiji kupata ajali ya basi ilipokuwa ikitoka mkoani Lindi baada ya mchezo dhidi ya Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.

MTIBWA ‘MBABE’ NYUMBANI NA UGENINI NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya Mtibwa Sugar inayoshikilia usukani wa Ligi ya Championship ya NBC imeendelea kuwa ‘Mwiba’ kwa timu za ligi hiyo kwa kushinda michezo mingi nyumbani na ugenini kuliko timu zote.

Mtibwa imeshinda michezo 11 nyumbani kwenye uwanja wa Manungu Complex, Morogoro huku ikishinda sita kwenye michezo yake ya ugenini na kuwa kinara wa ushindi nyumbani na ugenini.

Geita Gold inafuata ikiwa imeshinda michezo 10 kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita huku ikishinda minne ugenini sawa na timu za Mbeya Kwanza na Songea United.

Stand United ya Shinyanga na TMA FC ya Arusha zinashika nafasi ya tatu kwa kushinda michezo mingi kwenye uwanja wa nyumbani zikishinda michezo 9.