Author: Honest Mwanitega

LIGI KUU YA NBC KUTIMUA VUMBI LEO.

BAADA ya timu za KenGold, JKT Tanzania na Dodoma Jiji kuchukua alama tatu baada ya kushinda michezo yao hapo jana Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo mitatu itakayopigwa viwanja vitatu tofauti.

Mkoani Arusha timu ya Coastal Union iliyopoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa Azam kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa 10:00 alasiri.

Azam inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Mashujaa kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Zidane Sereri na Yoro Diaby.

Mkoani Kigoma timu ya Mashujaa iliyopoteza mchezo wake uliopita ugenini itakuwa mwenyeji wa timu ya Pamba Jiji ambayo imeshinda michezo mitatu mfululizo iliyopita bila kuruhusu bao katika michezo hiyo.

Mchezo wa mwisho utazikutanisha timu za Namungo itakayokuwa mwenyeji wa simba saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Mjaliwa, Lindi.

Timu ya Namungo inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ujao huku Simba ikihataji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.

SIMBA, DODOMA KUPANGIWA TAREHE MPYA LIGI KUU YA NBC.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeahirisha mchezo namba 148 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Simba SC na Dodoma Jiji ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa KMC Complex Februari 15, 2025 saa 10:00 alasiri.

Sababu ya kuahirishwa kwa mchezo huo ni baadhi ya wachezaji na maofisa wa ufundi wa klabu ya Dodoma Jiji kutokuwa katika hali nzuri kiafya baada ya basi la klabu hiyo walilokuwa wakisafiria kutoka Ruangwa mkoani Lindi, kupata ajali mkoani humo.

Ajali hiyo imesababisha athari hasi kwa klabu ya Dodoma Jiji kwa kuchelewesha safari yake ya kuelekea mkoani Dar es Salaam pamoja na kuathiri maandalizi ya kiufundi kwa kuwakosa wachezaji na maofisa wa ufundi ambao walipata majeraha katika ajali hiyo.

Ajali hiyo imepelekea Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuahirisha mchezo huo na itatangaza tarehe mpya hivi karibuni.

KMC YAREJEA NYUMBANI KIBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KMC ya Dar es Salaam imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza nyumbani dhidi ya Singida Black Stars kwa mabao 2-0 tangu kurejea kwa Ligi Kuu ya NBC iliyokuwa kwenye mapumziko mafupi.

Mabao mawili yaliyofungwa na Oscar Paulo kipindi cha kwanza yalitosha kuzamisha jahazi la Singida BS ambayo haijapata ushindi tangu kurejea kwa ligi hiyo.

KMC imefanikiwa kupata ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-1 huku Singida ikilazimishwa sare ya 2-2 mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar.

KMC imefikisha alama 22 na ‘kukwea’ hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku Singida BS ikisalia nafasi ya nne na alama 31.

DODOMA JIJI YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI.

TIMU ya Dodoma Jiji imepoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kurejea kutoka kwenye mapumziko mafupi kwa bao moja kutoka kwa Pamba Jiji ya mkoani Mwanza.

Mchezo huo uliokutanisha timu zilizopo chini ya manispaa za jiji ulipigwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kushuhudia bao lililofungwa kipindi cha kwanza na Mathew Tigisi likiizamisha Dodoma nyumbani.

Huu ni mchezo wa tatu kwa timu ya Pamba kushinda kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku ikishinda miwili ugenini na mmoja pekee ikishinda kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Dodoma imepoteza mchezo wa nane msimu huu idadi sawa na timu ya Pamba jiji huku Dodoma ikisalia nafasi ya tisa na alama 19 nne zaidi ya timu ya Pamba iliyofikisha alama 15 na kushika nafasi ya 14.

PRISONS YAIDUWAZA MASHUJAA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tanzania Prisons imerejea vema kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Mashujaa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mabao ya Prisons yalifungwa na Beno Ngassa mdogo wa nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania Mrisho Ngassa na Meshack Mwamita aliyefunga bao la ushindi kipindi cha pili huku bao la kufutia machozi kwa mashujaa likifungwa Seif Karihe kwa mkwaju wa penati.

Ukiwa mchezo wa kwanza kwa kocha mpya wa Prisons Amani Josiah kwenye Ligi Kuu ya NBC Prisons imesalia nafasi ya 13 ikifikisha alama 17 sawa na Namungo huku Prisons ikizidiwa kwa mabao ya kufunga.

Matokeo hayo yanaifanya timu ya Mashujaa kusalia nafasi ya saba ikiwa na alama 19 sawa na timu za JKT, Dodoma Jiji na KMC huku mashujaa ikiwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.