Author: Honest Mwanitega

KEN GOLD ‘HALI TETE’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KenGold kutoka mkoani Mbeya imeendelea kujiweka kwenye wakati mgumu wa kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kupoteza mchezo wa 14 wa ligi hiyo msimu huu dhidi ya Azam kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

KenGold inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC imepoteza mchezo wa 14 msimu huu na kuwa timu iliyofungwa michezo mingi sawa na timu ya Prisons ya Mkoani Mbeya pia.

Mabao ya Gibril Sillah na Nassor Saadun yalitosha kuipa Azam alama tatu muhimu huku golikipa Zuber Foba akimaliza mchezo bila kuruhusu bao na kufikisha idadi ya hati safi ‘Cleansheet’ ya tano msimu huu.

Azam imeendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu ikifikisha jumla ya alama 51 ikizidiwa alama sita pekee na Simba inayoshika nafasi ya pili na alama 10 nyuma ya kinara Yanga.

JKT YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya JKT Tanzania yenye ‘maskani’ yake uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na timu ya Dodoma Jiji.

Pamoja na kutangulia kupata bao kupitia kwa nahodha wake Edward Songo JKT ilishindwa kuizuia Dodoma iliyokuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara na kusawazisha mara zote JKT ilipotangulia kwa uongozi.

Mwana Kibuta aliinyima JKT uongozi hadi mapumziko baada ya kusawazisha bao la Songo zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya mapumziko.

Songo aliongeza bao la pili dakika ya 66 na kuipa JKT uongozi uliodumu kwa dakika 15 pekee kabla ya Paul Peter kuisawazishia Dodoma Jiji na kufanya matokeo kuwa 2-2 hadi mwisho wa mchezo.

Matokeo hayo yanaifanya JKT kushika nafasi ya sita na kuwa mbele ya Dodoma inayoshika nafasi ya saba kwa tofauti ya alama tatu.

PAMBA JIJI YABANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

IKICHEZA mchezo wa tano mfululizo timu ya Pamba Jiji imeshindwa kupata ushindi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya Namungo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Namungo ilikuwa ya kwanza kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Jacob Massawe huku Pamba ikisawazisha kupitia kwa Nyota Abdoullaye Camara anayecheza kwa mkopo kutokea timu ya Singida Black Stars huku likiwa bao lake la pili msimu huu.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba kushuka kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC hadi nafasi ya 13 ikiwa juu ya mstari wa kushuka daraja kwa tofauti ya alama tano.

Namungo imepanda hadi nafasi ya 12 baada ya kupata alama moja na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-26 chini ya kocha Juma Mgunda aliyewahi kufundisha timu za Coastal Union na Simba.

YANGA YAENDELEA ILIPOISHIA LIGI KUU YA NBC.

VINARA wa Ligi Kuu ya NBC Young Africans imeendelea kugawa ‘dozi’ inapocheza uwanja wa ugenini baada ya kuifunga Tabora United mabao 3-0 kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.

Mchezo wa jana umeshuhudia wachezaji wa Young Africans Prince Dube na Clement Mzize wakifunga bao moja kila mmoja na wote kufikisha mabao 11 msimu huu huku Israel Mwenda akifunga bao la pili msimu huu.

Huu ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Young Africans kushinda ugenini baada ya kuifunga Mashujaa 5-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na Pamba JIji 3-0 kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kwenye michezo hiyo Young Africans imefanikiwa kufunga mabao 11 na kufikisha jumla ya mabao 61 huku ikiwa imeruhusu mabao tisa na kuwa timu ya pili kuruhusu mabao machache msimu huu nyuma ya Simba iliyoruhusu mabao nane pekee.

MOUSSA CAMARA ANA JAMBO LAKE LIGI KUU YA NBC.

IKISALIA mizunguko saba kutamatika kwa Ligi Kuu ya NBC ‘Mlinda lango’ wa timu ya Simba Moussa Pinpin Camara ameendelea kushikilia usukani wa vinara ambao hawajaruhusu mabao kwenye ligi hiyo.

Camara hadi sasa amefikisha idadi ya michezo 15 aliyocheza bila kuruhusu nyavu zake kuguswa huku timu yake ikifungwa mabao nane pekee hadi sasa.

Golikipa huyo wa Simba amemzidi michezo minne mpinzani wake Djigui Diarra wa Yanga anayemfuatia kwa karibu akiwa amekusanya jumla ya michezo 11 bila kuruhusu bao.

Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa iliyoruhusu mabao 28 hadi sasa anashika nafasi ya tatu akiwa na michezo 10 bila kuruhusu bao huku idadi hiyo ikiwa sawa na golikipa wa Azam Mohammed Mustapha huku Azam ikiruhusu mabao 12 hadi sasa ikisalia na michezo saba kutamatisha msimu.