Author: Honest Mwanitega

YANGA YAENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

Timu ya Yanga imeendeleza ubabe inapocheza dhidi ya Simba baada ya kushinda kwa bao moja kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo kwenye uwanja wa Mkapa, Dar.

Bao la Yanga limepatikana baada ya mchezaji Kelvin Kijili kushindwa kuokoa mpira na kujifunga hivyo kufanya Yanga kushinda mchezo wa tano mfululizo msimu huu.

Hadi sasa Yanga ndio timu pekee ambayo haijaruhusu bao huku ikifunga mabao tisa na kuwa timu kinara wa wastani mzuri wa mabao sawa na timu ya Simba.

Kwa Matokeo hayo Yanga inapanda hadi nafasi ya pili ya msimamo ikikusanya jumla ya alama 15 nyuma ya kinara Singida Black Stars yenye alama 16 baada ya michezo sita.

KUFA AU KUPONA ‘KARIAKOO DERBY’ LIGI KUU YA NBC LEO.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaokutanisha ‘Miamba’ wa Tanzania kwenye soka timu ya Simba itakayokuwa nyumbani kuikaribusha Yanga kwenye uwanja wa Mkapa, Dar saa 11:00 jioni.

Huu ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu kwa timu hizo huku Simba ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa imetoka sare ya mabao mawili kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Timu ya Yanga itaingia kucheza ugenini leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuahinda mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya NBC kwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Pamba.

Yanga haijapoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu hadi sasa huku ikiwa na rekodi nzuri ya kushinda michezo yote iliyokutana na Simba msimu uliopita.

YANGA ‘MWENDO MDUNDO’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Yanga imepata ushindi wa bao moja dhidi ya KMC katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC.

Bao pekee la Yanga limefungwa na mchezaji Maxi Nzengeli dakika ya tano na kudumu mpaka mwisho wa mchezo huo hivyo kufanya KMC kupoteza mchezo wa tatu msimu huu.

KMC inaungana na timu za KenGold, na Tabora kuwa timu zilizofungwa mabao mengi msimu huu ikifungwa nane sawa na Tabora United huku KenGold ikifungwa mabao 10.

Yanga na Simba ndiyo timu pekee za Ligi Kuu ya NBC ambazo hazijaruhusu bao lolote hadi sasa.

SIMBA YAENDELEZA UBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Simba imeendeleza ubabe kwa timu inazokutana nazo baada ya kuifunga Dodoma Jiji bao moja kwenye uwanja wa Jmhuri, Dodoma.

Huu ni ushindi wa nne mfululizo kwa timu ya Simba ikifanikiwa kufunga mabao 10 huku ikiwa haijaruhusu bao lolote mpaka sasa.

Dodoma imepoteza mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC, ikipata sare tatu na kusalia na alama sita kwenye nafasi ya 10.

Simba ni timu ya pili kwa kufunga mabao hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC ikifunga 10 nyuma ya timu ya Fountain Gate ya Babati iliyofunga mabao 12 hadi sasa.

MASHUJAA, AZAM HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Mashujaa ya Kigoma imeshindwa kutakata kwenye uwanja wa Lake Tanganyika baada ya kulazimishwa suluhu na timu ya Azam.

Hii ni sare ya pili mfululizo kwa timu ya Mashujaa iliyofikisha alama tisa na kukwea hadi nafasi ya sita baada ya kucheza michezo mitano.

Azam imeshindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa pili mfululizo baada ya kupoteza mchezo uliopita kwa mabao 0-2 nyumbani dhidi ya Simba.

Hii ni sare ya kwanza kwa Azam inayowafanya kufikisha alama tisa baada ya kucheza michezo sita na kukaa nafasi ya tano ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.