Author: Honest Mwanitega

SINGIDA YABANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Singida Black Stars imepata sare ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya kutoka 1-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Singida iliyoshinda michezo minne mfululizo ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa Elvis Rupia mapema kipindi cha kwanza kabla ya Wilson Nangu kusawazisha kwenye kipindi cha pili.

Hii ni sare ya nne kwa timu ya JKT Tanzania ikiungana na timu za Tanzania Prisons na Pamba kuwa timu zenye sare nyingi kwenye Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa.

Sare hiyo inaifanya Singida kufikisha alama 13 sawa na Fountain Gate huku Singida ikiongoza Ligi Kuu ya NBC kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC KUANZA LEO.

MSIMU mpya wa Ligi ya Championship ya NBC unatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo kwa michezo miwili itakayopigwa kwenye mikoa miwili tofauti.

Michezo yote inatarajiwa kuanza saa 10:00 alasiri, Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Bigman FC kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya huku Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC itakuwa mwenyeji wa Green Warriors kwenye uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.

Ligi hiyo itaendelea tena Septemba 21, kwa michezo mitatu itakayopigwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Songea United itaialika Mbeya Kwanza kwenye uwanja wa MajiMaji, Ruvuma huku Cosmopolitan ikiialika African Sports kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro na mchezo wa mwisho utapigwa kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita kati ya Geita Gold na TMA ya Arusha.

AZAM YAITOLEA UVIVU KMC LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Azam FC imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC baada ya kuifunga mabao 0-4 kwenye uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam.

Bao la kwanza la Azam msimu huu limefungwa na Iddy Seleman kwenye mchezo huo dhidi ya KMC huku mabao mengine yakifungwa na Lusajo Mwaikenda, Nassor Saadun na Nathaniel Chilambo huku golikipa wa Azam Zubeir Foba akimaliza mchezo wake wa pili bila kuruhusu bao.

Matokeo hayo yanaipeleka Azam hadi nafasi ya sita ya Ligi Kuu ya NBC ikifikisha alama tano baada ya kucheza michezo mitatu huku KMC ikiwa na alama nne kwenye nafasi ya nane ya msimamo.

Ligi hiyo inaendelea leo kwa michezo miwili itakayopigwa kwenye mikoa miwili tofauti huku mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, Tabora kati ya Tabora United na Fountain Gate huku mchezo wa mwisho ukipigwa kwenye uwanja wa Kaitaba saa 1:00 usiku, Kagera kati ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya 15 na KenGold inayoshika nafasi ya 16 ikiwa haijapata alama yoyote hadi sasa.

PAMBA, SINGIDA KUKIWASHA MWANZA, COASTAL KUJIULIZA LIGI KUU YA NBC.

BAADA ya KMC kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC jana dhidi ya KenGold kwa bao moja huku Kagera Sugar ikitoka suluhu na JKT Tanzania leo ligi hiyo inaendelea kwa michezo miwili.

Mapema saa 8:00 mchana timu ya Pamba ya Mwanza itakuwa mwenyeji wa Singida BS kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Pamba haijaruhusu bao mpaka sasa huku ikitoa suluhu kwenye michezo yake mitatu iliyocheza dhidi ya Prisons, Dodoma Jiji na Azam FC huku timu ya Singida ikishinda michezo yote mitatu iliyocheza na KenGold, Kagera Sugar na KMC.

Saa 10:15 alasiri Coastal Union ambayo haijapata ushindi wowote msimu huu itakuwa uwanja wa nyumbani Azam Complex dhidi ya Namungo iliyopoteza michezo yote ya Ligi Kuu ya NBC hadi sasa.

COASTAL KUJIULIZA KWA MASHUJAA LEO KWENYE LIGI KUU YA NBC.

BAADA ya Singida Black Stars na Dodoma Jiji kutamba kwenye uwanja wa nyumbani jana kwa ushindi jana timu ya Coastal Union leo itakuwa mwenyeji wa Mashujaa kuzisaka alama tatu muhimu.

Coastal iliyochagua kutumia uwanja wa KMC uliopo Dar kama uwanja wa nyumbani kwenye mchezo huu itacheza huku ikipambana kupata ushindi wa kwanza msimu huu dhidi ya Mashujaa ambayo haijapoteza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Coastal ilipata sare ya bao moja kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya KMC baada ya Maabad Maabad kusawazisha dakika za mwisho kwa mkwaju wa penati.

Mashujaa ni miongoni mwa timu saba za Ligi Kuu ya NBC ambazo bado hazijaruhusu bao lolote msimu huu ikiungana na timu za Simba, Yanga, Pamba Jiji, Azam, Tanzania Prisons na JKT Tanzania.