Author: Loveness Bernard

YOUNG AFRICANS ‘HAWACHEKESHI’ NDANI YA BOKSI

UTAMU wa Ligi Kuu ya NBC unazidi kukolea ikiwa ni mzunguko wa 27 wa Ligi hiyo huku timu ya Young Africans ikiongoza kwa kufunga mabao mengi ndani ya eneo la boksi (18).

Young Africans imefanikiwa kufunga mabao  55 ndani ya boksi ikiwa ni mabao mengi kufungwa na timu kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Simba nayo haina mzaha ikiwa ndani ya boksi ambapo hadi sasa ikifanikiwa kufunga mabao 48  huku Azam ikiwa na mabao 38 kwenye eneo hilo la 18.

Singida Black Stars nayo haina utani iwapo wachezaji wake wakipata mpira ndani ya boksi ikiwa imeshafunga mabao 37 huku Tabora United na Dodoma Jiji zikiwa na mabao 23.

Kwa upande wa Namungo imefanikiwa kufunga mabao 22 na Fountain Gate ikifunga mabao 20 ndani ya eneo hilo la 18.

LIGI KUU YA NBC KUREJEA MEI 2

LIGI Kuu ya NBC, Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika  itarejea Mei 2 kwa mchezo kati ya Simba itakayokuwa mwenyeji wa timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma.

Mchezo huo utachezwa katika uwanja wa KMC Complex uliopo mkoani Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa mzunguko wa 24 uliosogezwa kutokana na timu ya Simba kuwa na ratiba ya michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya mchezo huo timu ya Simba itakuwa na kibarua kingine ugenini katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar watakapokutana na timu ya JKT Tanzania waliyoifunga 1-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa bao la Jean Ahoua aliefunga kwa mkwaju wa penati dakika za nyongeza.

Mei 8 itaikaribisha timu ya Pamba katika uwanja wa KMC Complex kabla ya kwenda ugenini kuvaana na timu ya KMC kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

MTIBWA YAPANDA RASMI LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mtibwa Sugar imepanda rasmi Ligi Kuu ya NBC ambayo ni Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika  wakitokea Ligi ya Championship ya NBC baada ya kufanikiwa kufikisha alama 67 ambazo hakuna timu itaweza kuzifikia  katika michezo 28 abayo timu hiyo imeshacheza mpaka sasa.

Mtibwa ambayo ilishuka daraja msimu uliopita na sasa wamerejea rasmi huku ikiwa imeweka rekodi ya kucheza michezo 14 katika uwanja wao wa nyumbani wa Manungu pasipo kufungwa huku michezo 14 ya ugenini wakishinda saba kupata sare nne na kufungwa michezo mitatu.

Aidha timu hiyo imefanikiwa kufunga mabao 54 kuruhusu mabao 16 katika michezo timu hiyo  iliyocheza huku wakiwa wamebaki na michezo miwili ili kuweza kutamatika kwa Ligi ya Championship ya NBC

LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC YABAKIZA MIZUNGUKO MITATU

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inautaarifu umma kuwa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025 inaingia kwenye mzunguko wa 28 leo Jumamosi Aprili 26, 2025 ambapo kila klabu imesaliwa na michezo mitatu tu kabla ya kumaliza msimu.

Bodi ilipanga na kutangaza kuwa michezo yote ya kila mzunguko uliosalia itachezwa katika tarehe na muda mmoja kwa lengo la kuongeza usawa kwenye ushindani baina ya timu shiriki.

Kwasababu inafahamika kuwa ushindani na msukumo umeongezeka zaidi katika kipindi hiki klabu zinafanya jitihada za kutimiza malengo yao ya msimu, Bodi imeongeza nguvu katika usimamizi wa michezo hiyo ili msukumo huo uzae burudani viwanjani badala ya kusababisha uvunjifu wa Kanuni za Ligi na sheria za mpira wa miguu.

Ni wajibu wa kila mdau wa Ligi hiyo kuhakikisha anafuata Kanuni za Ligi ikiwemo kujiepusha na kukumbusha wengine kutojihusisha na vitendo vyovyote vinavyoashiria upangaji wa matokeo.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania itachukua hatua kali za kinanuni kwa kila mdau atakayebainika na kuthibitika amejihusisha kwa namna yoyote na upangaji wa matokeo kwasababu jambo hilo ni katika mambo yanayoweza kushusha hadhi ya Ligi.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inawatakia kila la kheri wadau wote wa Ligi hiyo kuelekea michezo iliyosalia.

VIWANJA NANE ‘KUWAKA MOTO’ LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP KESHO

LIGI ya NBC Champioship inaendelea kushika kasi ikielekea mwishoni  na  hapo kesho michezo nane ya mzunguko wa 28 itachezwa katika viwanja mbalimbali nchini majira ya saa kumi jioni .

Timu ya Cosmopolitan ambayo iko nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC itaikaribisha timu ya Stand United iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Green Warriors iliyopo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi ya Champioship itaikaribisha timu ya Biashara United ambayo ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo mchezo utakaochezwa uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Transit Camp  ikiwa kwenye nafasi  ya 14 katika msimamo itaikaribisha timu  ya TMA  iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo mchezo utakaochezwa katika uwanja wa TFF Centre uliopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Timu ya Kiluvya iliyopo nafasi ya 12 itaikaribisha timu ya  Mbuni ambayo iko nafasi ya tisa katika mchezo utakaochezwa uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Mbeya Kwanza  iliyo nafasi ya sita itachuana  vikali na African Sports iliyo nafasi ya 15 mchezo utakaochezwa uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.

Timu ya Bigman iliyo nafasi ya saba itawaalika timu ya Mtibwa Sugar inayoongoza Ligi ya Championship ya NBC katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Wachimba madini yaani Geita Gold iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo itawakaribisha Mbeya City iliyo nafasi ya pili katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita huku Songea United iliyopo nafasi ya nane ikiwakaribisha Polisi Tanzania iliyo nafasi ta 10  katika uwanja wa Majimaji mkoani Songea.