Author: Loveness Bernard

SIMBA ‘KUKIWASHA’ NA MASHUJAA LEO LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inarejea rasmi leo ambapo mchezo mmoja utachezwa katika uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge mkoani Dar es Salaam timu ya Simba ikiikaribisha timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma.

Mchezo huo utachezwa majira ya saa kumi jioni ikiwa ni mchezo wa kiporo cha mzunguko wa 24 wa Ligi Kuu ya NBC ambao haukuchezwa kutokana na Simba kuwa na michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo wamefanikiwa kufuzu fainali ya michuano hiyo.

Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 57 ikifanikiwa kufunga mabao 52 na kuruhusu mabao 8 ikiwa ni timu iliyoruhusu mabao machache kuliko timu zote ikiwa timu hiyo imeshacheza michezo 22.

Mashujaa ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefanikiwa  kufunga mabao 26 ikiruhusu mabao 30 katika michezo 26 ambayo timu hiyo imeshacheza.

MBEYA CITY YAREJEA LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mbeya City imerejea rasmi Ligi Kuu ya NBC ambayo ni Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika  wakitokea Ligi ya Championship ya NBC baada ya kufanikiwa kufikisha alama 65 baada ya kuifunga timu ya Cosmopolitan mabao 5-0 huku ikiwa na mchezo mmoja ikiwa ni wiki moja baada ya Mtibwa Sugar kufanikiwa kurejea Ligi Kuu ya NBC.

Mbeya City ilishuka  na sasa wamerejea rasmi huku ikiwa imeweka rekodi ya kufunga mabao mengi ksatika Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 63 katika michezo 29 ambayo timu hiyo imeshacheza mpaka sasa huku katika michezo yao  14 ya nyumbani wakishinda 11 na sare 3 na ugenini  michezo 15 wakishinda michezo nane sare tano na kufungwa michezo miwili

 

Aidha timu hiyo imefanikiwa kufunga mabao 63 kuruhusu mabao 26 katika michezo timu hiyo  iliyocheza huku wakiwa wamebaki na mchezo mmoja ili kuweza kutamatika kwa Ligi ya Championship ya NBC ambao pia utaamua nani bingwa wa Ligi hiyo kati ya Mtibwa Sugar wenye alama 68 au Mbeya City wenye alama 65.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA USULUHISHI WA MICHEZO CAS YATUPILIA MBALI RUFANI YA YOUNG AFRICAN

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imetupa rufani ya klabu ya Yanga yenye kumbukumbu namba CAS 2025/A/11298 ambayo klabu hiyo iliifungua dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC).

Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ambapo pamoja na mengine, klabu ya Yanga iliomba mechi tajwa hapo juu isipangiwe tarehe mpaka litakapotolewa uamuzi, ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), na klabu ya Simba.

Kutokana na uamuzi huo wa CAS, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaendelea na maandalizi yake ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2024/2025 na kufanya maboresho ya ratiba ya Ligi (ukiwemo mchezo namba 184 – Young Africans vs Simba SC) kisha kutangaza ratiba mpya mapema iwezekanavyo.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Aprili 26, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Timu ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya imepewa adhabu ya Onyo Kali kwa kosa la wawakilishi wa timu kuchelewa kwa dakika 12 kuwasili kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2 (2.1).Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 194: Tanzania Prisons 1-0 Kagera Sugar

Klabu ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la watoto waokota mipira (Ball Kids) kuficha na kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani.

Kuanzia dakika ya 63 ya mchezo, watoto hao walikuwa wakificha mipira inayotoka hali iliyosababisha hadi kufika dakika ya 80 ya mchezo uwe umesalia mpira mmoja pekee kiwanjani.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 195: Pamba Jiji 1-0 Tabora United

Klabu ya Tabora United ya mkoani Tabora imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kwa kile walichoeleza kuwa kulikuwa na harufu isiyo ya kawaida.

Kamishna pamoja na Mratibu wa mchezo huo waliwasiliana na Daktari wa mchezo ili kuthibitisha hali hiyo lakini aliwaeleza kuwa harufu hiyo ilikuwa ya Sabuni zilizotumika kufanyia usafi katika vyumba vyote (kikiwemo chumba cha timu mwenyeji).Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 200: Singida BS 1-0 Azam FC

Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC Rachid Taoussi ameadhibiwa kwa kutozwa faini yaSh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwafanyia vurugu na kuwarushia chupa ya maji waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu mara baada ya mchezo huo kutamatika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Mechi Namba 202: Pamba Jiji 1-1 Fountain Gate

Klabu ya Fountain Gate imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kwa kile walichoeleza kuwa chumba hicho kilikuwa na joto, uamuzi ambao waliufanya bila kumshirikisha Afisa yeyote wa mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 195: Green Warriors 2-3 Polisi Tanzania

Klabu ya Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro imeadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo. Meneja wa timu ya Polisi Tanzania Maliki Warioba alifika kwenye kikao saa 4:25 huku viongozi wengine wakifika saa 4:35 badala ya saa 4:00 ambapo walikuta kikao kimefungwa.

Kuchelewa kwenye Kikao cha Maandalizi ya mchezo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo.

Mechi Namba 201: Kiluvya FC 0-1 Mbeya Kwanza

Klabu ya Mbeya Kwanza ya mkoani Mtwara imeadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne (4) badala ya watano (5) kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo

Mechi Namba 203: Mtibwa Sugar 2-1 Mbuni FC

Klabu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imeadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali kwa kosa la maofisa wake wawili kutokuvaa sare za timu kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.10) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo

Mechi Namba 207: Songea United 1-2 Stand United

Klabu ya Songea United ya mkoani Ruvuma imeadhibiwa kwa kupewa Onyo kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani. Songea United waliwasili uwanjani saa 8:45 mchana badala ya saa 8:30 mchana kinyume na kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo

Mechi Namba 214: Geita Gold 2-1 Songea United

Klabu ya Songea United ya mkoani Ruvuma imeadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo. Wawakilishi timu ya Songea United walifika kwenye kikao saa 4:07 badala ya saa 4:00.Kuchelewa kwenye Kikao cha Maandalizi ya mchezo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo.

First League

Mechi Namba 54A: Pan African 1-1 Nyumbu FC

Daktari wa klabu ya Nyumbu, Alex Theodory amefungiwa kwa kipindi cha mwezi moja (1) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kumtolea lugha ya matusi mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu.

Daktari huyo alifanya kitendo hicho kisicho cha kiuanamichezo wakati wa mchezo huo na aliadhibiwa pia kwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:3 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

Mechi Namba 56A: Dar City 3-0 Tunduru Korosho

Klabu ya Tunduru Korosho ya mkoani Ruvuma imeadhibiwa kwa kupewa Onyo Kali kwa kosa la wawakilishi wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo. Kutokufika kwenye Kikao cha Maandalizi ya mchezo ni kwenda kinyume na Kanuni ya 18:2 (2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za mchezo.

Mechi Namba PO1: Tunduru Korosho 2-2 Mapinduzi FC

Meneja wa klabu ya Mapinduzi, David Kinasa amefungiwa kwa kipindi cha mwezi moja (1) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kumtolea lugha ya matusi mwamuzi wa mchezo.

Kinasa alifanya kitendo hicho kisicho cha kiuanamichezo wakati wa mchezo huo na aliadhibiwa pia kwa kadi nyekundu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:3 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

 

 

MBEYA CITY WAKALI WA ‘KUTUPIA’ NBC CHAMPIONSHIP

TIMU ya Mbeya City imeendelea kuongoza kwa kufunga mabao kuliko timu yoyote katika Ligi ya Championship ya NBC licha ya kuwa katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi hiyo.

Mbeya City wamefanikiwa kufunga mabao 58 katika michezo 28 ambayo timu hiyo imecheza huku ikiwa imeruhusu mabao 26 na kukusanya alama 62 ikiwa nafasi ya pili katika msimamo nyuma ya Mtibwa Sugar ambayo imeshapanda Ligi Kuu ya NBC.

Mtibwa Sugar wanafuatia kwa kufunga mabao ikifunga mabao 54 na kuruhusu mabao 16 katika michezo 28 iliyocheza huku ikiwa imekusanya alama 67 na ikiongoza katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Geita Gold imefanikiwa kufunga mabao 49 huku ikiruhusu mabao 24 pamoja na kuvuna alama 54 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo huku Stand United ikifunga mabao 47 na kuruhusu  mabao 23 wote wakiwa  wamecheza michezo 28 katika Ligi hiyo.

Mbeya Kwanza imefunga mabao 40 baada ya kucheza michezo 28 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26 na ikiwa nafasi  ya sita katika mbio za ubingwa wa Ligi hiyo.