Author: Loveness Bernard

DUBE,AHOUA HAPATOSHI UFUNGAJI BORA LIGI KUU NBC.

VITA ufungaji bora imeanza upya ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wa Young Africans Prince Dube kumfikia  idadi ya mabao kiungo wa Simba,Jean Ahoua huku Ligi Kuu ya NBC ambayo ni Ligi namba nne kwa ubora barani Africa ikielekea ukingoni.

Dube ambaye amefunga mabao 12 na kutoa pasi za mwisho nane katika michezo 25 ambayo timu yake imeshacheza mpaka sasa katika Ligi Kuu ya NBC sawa na Ahoua wa timu ya Simba ambaye amefanikiwa kufunga mabao 12  na kutoa pasi za mwisho saba katika michezo 22 ambayo timu yake imeshacheza.

Young Africans imebakisha michezo mitano ikiwa imeshacheza michezo 25 huku Simba ikiwa imebakisha michezo minane baada ya kucheza mechi 22 hivyo njia inaweza kuwa nyepesi kwa wachezaji hao na wengine wanaowakaribia kuibuka na ufungaji bora wa Ligi Kuu mara baada ya kufikia ukingoni.

 

COASTAL UNION WAIZINDUA MKWAKWANI KIBABE LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea kushika kasi ambapo jana Coastal Union iliwakaribisha timu ya Singida Black Stars katika uwanja wa Mkwakwani Tanga ikiwa ni mechi ya kwanza tangu kuboreshwa kwa uwanja huo.

Mchezo huo ulianza majira ya saa 10:00 alasiri ambapo timu zote zilikuwa na shauku ya kuchukua alama ili kujiweka katika mazingira mazuri Coastal Union wakiendelea kujinasua kutoka nafasi za chini kwenye msimamo na Singida wakipambania nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Dakika 47 ziliwatosha Coastal Union kuongoza mchezo baada ya kupata bao la kwanza baada ya mchezaji wa Singida Josephat Bada kujifunga hivyo kuwafanya wana mangushi kwenda mapumziko na uongozi wa 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 76 mshambuliaji wa Singida, Jonathan Sowah aliipatia timu yake bao kupitia mkwaju wa penati na dakika ya 82 mchezaji wa Coastal union, Bakari Msimu aliongeza bao hivyo mchezo kutamatika kwa 2-1.

Matokeo hayo yanaipeleka Coastal hadi nafasi ya 10 na alama 28 huku Singida ikisalia nafasi ya nne ikiwa na alama 50.

YOUNG AFRICANS WABABE WA DABI YA DAR

LIGI Kuu ya NBC imeendelea jana ambapo mchezo wa Dabi ya Dar es Salaam ambapo Azam iliwakaribisha Young Africans uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex majira ya saa moja usiku.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa huku Young Africans wakionekana kushambulia kwa kasi kubwa  huku Azam wakionekana kuzuia kwa kasi ya wapinzani wao.

Ilimchukua dakika 11 tu kiungo wa Young Africans Pacome Zouzoua  kufungua ukurasa wa mabao ambapo aliitanguliza timu yake huku Prince Dube akiongeza bao dakika ya 34 ya mchezo huo  na kufanya timu hiyo kwenda mapumziko wakiwa wako mbele kwa mabao 0-2.

Kipindi cha pili mchezo uliendelea kwa timu zote kusaka mabao ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi na dakika ya 81 beki wa Azam Lusajo Mwaikenda alifungua ukurasa wa mabao kwa timu yake hivyo kufanya mchezo kuwa wa kasi ya kushambuliana zaidi ambapo dakika 90 zilitamatika kwa matokeo ya 1-2.

Mshambuliaji wa Young Africans Prince Dube alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuisaidia timu yake kupata ushindi.

 

PACOME AIBEBA YANGA IKIIFUNGA COASTAL LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa KMC Complex ambapo timu ya  Young Africans iliikaribisha timu ya Coastal Union  kutoka Tanga.

Mchezo huo ulianza majira ya saa kumi na robo jioni ambapo timu zote zilikuwa zikishambuliana huku pia zikiimarisha ulinzi katika lango lao ili kutokuruhusu bao lolote.

Ilimchukua dakika 34 mchezaji wa Young Africans Pacome Zouzoua kufungua ukurasa wa mabao hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza ambapo timu zote zilionekana zikitaka alama  tatu  muhimu ambapo hata hivyo mchezo  ulitamatika kwa Young Africans kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Youn Africans imezidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa baada ya kufikisha alama 64 huku wakiwa wamecheza michezo 24  na wakiendelea kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu  huku timu ya  Coastal Union ipo nafasi ya13  katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 25.

 

 

 

KASEJA AIFUFUA UPYA KAGERA SUGAR

TIMU ya Kagera Sugar imeanza kujipata katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC baada ya kushinda mechi tatu walizocheza hivi karibuni chini ya uongozi wa Kocha wao mpya Juma Kaseja ambaye pia ni golikipa aliyecheza kwa mafanikio makubwa timu ya taifa na timu mbalimbali za Ligi Kuu .

Kaseja ambae alichukua mikoba kutoka kwa Kocha Melis Medo ambae ametimkia katika timu ya Singida Black Stars  aliiongoza timu yake katika mchezo miwili huku mchezo wa kwanza  dhidi ya Pamba Jiji  alifanikiwa kushinda mabao 2-1.

Mchezo mwingine ulichezwa jana April 3 alifanikiwa kuifunga timu ya Coastal Union kwa mabao 2-1 ambapo mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Ally Msangi wa Coastal Union aliyejifunga bao  dakika ya 59 na Mohamed Jecha dakika ya 90  huku mchezaji Lucas Kikoti akiipatia Coastal Union bao dakika ya 84 ya mchezo huo.

Kagera Sugar imefikisha alama 22 ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 24 wakifunga mabao 20 na kufungwa mabao 32.