Author: Loveness Bernard

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Agosti 21, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 001: Pamba Jiji 1-1 Dodoma Jiji

Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji wake kuonekana wakifanya kitendo kinachoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo tajwa hapo juu.Wakati wa kufanya mazoezi Wachezaji hao walijikusanya Katikati ya uwanja na kuweka duara kuashiria kuomba dua lakini mmoja kati ya wachezaji hao alionekana akichimbia vitu chini.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Klabu ya Pamba Jiji imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuelekea mchezo tajwa hapo juu Agosti 14, 2026.Pamba iliwasili uwanjani saa 6:51 Mchana badala ya saa 6:30 Mchana jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 0010: Namungo 1-0 Geita Gold

Klabu ya Namungo imepewa onyo kali kwa kosa la vijana waokota mipira (Ball Boys) kuficha mipira na wakati mwingine kutoifata kabisa pindi mipira hiyo ilivyotoka nje. Kitendo hicho si cha kiungwana na kiuanamichezo, Kamati inatoa angalizo kwa klabu zote kuheshimu na kuzingatia kanuni ya Uchezaji wa Kiungwana.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 0012: Pamba Jiji 1-2 Simba SC

Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakati wa mapumziko hali iliyofanya waamuzi hao kushindwa kutumia vyumba vya kubadilishia nguo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mchezaji wa Simba Ibraheem Jabaar ametozwa faini ya Sh 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji jezi namba 35 (Abdulkarim Iddy) pamoja na hiyo, adhabu ya kadi nyekundu itaendelea kubaki kama ilivyo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 0013: Kagera Sugar 1-1 Singida BS

Mchezaji wa Singida BS Mathew Tegisi amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Kagera Sugar jezi namba 12 (Salehe Seif).

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Tatu Malogo kutoka Tanga amepewa Onyo Kali kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

 TAARIFA MAALUM

Kamati inazikumbusha timu zote kuzingatia kikamilifu masharti ya Kanuni ya 20 kuhusu Matumizi ya Teknolojia ya Football Video Support System (FVS).Kwa mujibu wa Kanuni ya 20(4), ni Kocha Mkuu au kiongozi mwingine wa juu kwenye benchi la ufundi pekee mwenye haki ya kuwasilisha ombi la marejeo ya tukio katika FVS, kwa kuwasiliana na Mwamuzi wa Akiba (Fourth Official).

Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 20(4)4.1, iwapo mchezaji ataona tukio linahitaji marejeo ya FVS, anatakiwa kuwasiliana kwa ishara na Kocha Mkuu au kiongozi wa benchi la ufundi, ambaye ndiye atakayewasilisha ombi hilo.

Ni marufuku kwa mchezaji kumkabili, kumlalamikia au kumshinikiza mwamuzi moja kwamoja kwa lengo la kuomba marejeo ya FVS. Mchezaji atakayekiuka masharti hayo ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.

Kamati itaendelea kusimamia utekelezaji wa kanuni hizi, na adhabu zitatolewa dhidi ya watakaobainika kukiuka masharti yaliyowekwa.

 SIMBA YAJIPATA KAGERA, JKT, TRA ZAIDI YA MCHEZO.

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC umetamatika jana kwa michezo miwili iliyopigwa mkoani Kagera na Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza ulichezwa uwanja wa Kaitaba ambapo timu ya Kagera Sugar ilikuwa mwenyeji wa timu ya Simba mchezo uliochezwa majira ya saa kumi jioni.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikiwa na ari kubwa ya kutaka alama tatu muhimu ili kuanza vyema katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa Kagera Sugar imerejea baada ya kucheza Championship msimu uliopita na kushika nafasi ya pili.

Ilimchukua dakika 45 beki wa Simba Ismail Traore kufungua ukurasa wa mabao baada ya kuruka na kufanikiwa kufunga bao la kichwa na timu zilienda mapumziko 0-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Kagera Sugar ikitaka kusawazisha huku Simba ikitaka kuongeza bao ambapo dakika ya 68 Elie Mpanzu aliongezea bao timu yake hivyo mchezo kutamatika kwa 0-2 na kiungo wa Simba Libase Gueye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa pili ulikuwa kati ya JKT Tanzania dhidi ya TRA United ulichezwa katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo majira ya saa mbili na nusu usiku.

Kipindi cha kwanza kilianza huku TRA wakitawala mchezo kwa dakika zote 45.

Dakika 13 pekee zilimtosha Tobias Omondi wa TRA kufungua ukurasa wa mabao ambapo mchezo huo ulienda mapumziko kwa 0-1.

Kipindi cha pili JKT Tanzania walionekana wakitawala mchezo ambapo dakika ya 50 walisawazisha kupitia mchezaji wao Godfrey Luzendaze na matokeo yalisalia 1-1 mpaka mchezo unatamatika huku mchezaji wa TRA Joseph Akandwanaho alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

YOUNG AFRICANS YATAKATA KUSINI MWA TANZANIA.

TIMU ya Young Africans imeanza vema kampeni ya kutetea ubingwa wake baada ya kuifunga Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa uwanja wa Majaliwa, Ruangwa jana.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku Young Africans wakionyesha kuzitaka alama tatu na walifanikiwa kutawala mchezo huo ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinatamatika hakuna ambaye alifanikiwa kuingia katika lango la mwenzake .

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa timu zote zikisaka bao na dakika ya 68 Chadrack Boka wa Young Africans alianza kufungua ukurasa wa mabao huku Max Nzengeli akifunga bao la pili dakika ya 71 ya mchezo huo.

Namungo ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 75 na kuweza kumuharibia kipa wa Young Africans Djigui Diarra hati safi yake ya kwanza kwa msimu wa 2026/2027.

POLISI, AZAM WAGAWANA ALAMA ARUSHA.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kushika kasi ambapo timu ya Polisi Tanzania iliikaribisha timu ya Azam katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana.

Mchezo huo ulichezwa majira ya saa kumi jioni ambapo ulikuwa muhimu kwa timu zote ikiwa ni mchezo wa kwanza wa msimu wa 2026/2027 hivyo timu zote zilitaka ushindi ili kuanza vyema msimu.

Mchezo ulianza kwa kasi kubwa huku timu zote zikishambuliana na kujilinda kuhakikisha hawaruhusu mpinzani kuingia katika lango lao na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna aliyefanikiwa kuingia katika lango la mwenzake.

Timu zilirejea na kasi kubwa ya kutafuta ushindi na dakika ya 79 Abdul Suleman wa Azam aliitanguliza mbele timu yake kupitia mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa Azam kufanyiwa madhambi ambapo mwamuzi Hance Mabena alijiridhisha kupitia mfumo mpya wa kusaidia waamuzi (Football Video Support (FVS) na kutoa maamuzi.

Anuary Jabir wa Polisi Tanzania aliwanyanyua maafande hao baada ya kufunga bao la kusawazisha kupitia mkwaju wa penati pia baada ya mchezaji wa Polisi Tanzania kuchezewa madhambi na mwamuzi kujiridhisha kupitia FVS hivyo mchezo ulitamatika kwa timu hizo kugawana alama 1-1.

LIGI KUU YA NBC MSIMU WA 2026/27 KUANZA LEO.

Pazia la Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027 linafunguliwa rasmi leo kwa michezo mitatu itakayochezwa katika viwanja mbalimbali nchini.

Mchezo wa kwanza utakuwa jijini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba majira ya saa nane mchana ambapo timu ya Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa timu ya Dodoma Jiji huku mchezo huo ukitarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na timu zote mbili kutaka alama hizo ili kuanza kujiweka katika nafasi nzuri.

Mchezo wa pili utakuwa jijini Mbeya katika uwanja wa Sokoine ambapo timu ya Mbeya City itakuwa mwenyeji wa timu ya Geita Gold iliyorejea Ligi Kuu baada ya kuwa mabingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita mchezo huo utakuwa majira ya saa kumi na robo jioni.

Mchezo wa mwisho utakuwa majira ya saa moja jioni ambapo timu ya Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa timu ya Fountain Gate katika uwanja wa Airtel mkoani Singida.