Author: Loveness Bernard

LIGI KUU YA NBC YAREJEA.

LIGI Kuu ya NBC inarejea leo kwa michezo mitatu itakayochezwa Dar es Salaam, Arusha na Tanga baada ya mapumziko ya takribani wiki mbili kupisha michezo ya kalenda ya FIFA.

Michezo miwili ya kwanza itapigwa majira ya saa kumi jioni mkoani Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo timu ya Fountain Gate iliyopo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Lgi Kuu ya NBC itaikaribisha timu ya Azam iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Mchezo mwingine utakaopigwa muda huo ni kati ya Coastal Union iliyopo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Lgi Kuu ya NBC itakuwa mwenyeji wa timu ya Namungo iliyopo nafasi ya 13 katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Mchezo wa mwisho utakuwa jijini Dar es Salaam ambapo KMC iliyopo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Lgi Kuu ya NBC itaikaribisha timu ya TRA katika uwanja wa KMC Complex majira ya saa mbili usiku ukiwa ni mchezo wa mwisho wa kukamilisha siku.

OKELLO, BARKER WANG’ARA TUZO MEI.

KIUNGO mshambuliaji  wa Young Africans, Allan Okello, amechaguliwa kuwa mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku Steve Barker wa Simba  akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Mchezaji wa Young Africans, Allan Okello.

Okello alionyesha kiwango kizuri chenye mwendelezo kwa mwezi huo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao tisa na kuhusika na lingine moja kwa kutoa pasi ya usaidizi  katika dakika 509 za michezo sita, ambayo Young Africans ilicheza nakuisaidia kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezaji huyo aliwashinda viungo Clatous Chama wa Simba na Feisal Salum wa Azam alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker.

Kwa upande wa Barker aliyeingia fainali na Florent Ibenge wa Azam na Fred Minziro wa Fountain Gate, aliiongoza timu yake kushinda michezo mitanoi liyocheza na kutoka sare mmoja na kuendelea kubaki nafasi ya pili kwenyemsimamo wa ligi.

Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Airtel Singida, Omar Malule amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Mei kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Katika hatua nyingine Salum Mlemwa wa Gunners amechaguliwa Mchezaji Bora waMwezi Mei wa Ligi ya NBC Championship 2025/26, huku Henry Mkanwa pia waGunners akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Mlemwa aliyeingia fainali na Richardson Ng’ondya wa Geita Gold na Maulid Shaaban wa Geita Gold, alionyesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne kwa dakika  357  za michezo mitano aliyocheza.

Kwa upande wa Mkanwa aliyeingia fainali na Twaha Beimbaya wa B19 na Mbwana Makata wa Polisi Tanzania, aliiongoza timu yake kushinda michezo yote minne iliyocheza na kupaa kutoka nafasi ya 11 hadi ya saba kwenye msimamo wa Ligi yaChampionship ya NBC.

Pia Kamati ya Tuzo iliteua mabao matatu bora yatakayopigiwa kura na mashabikiili kupata bao bora la mwezi. Mabao hayo ni la Paul Peter (JKT Tanzania vs Fountain Gate dakika ya 85), Clatous Chama (Simba SC vs Young Africans, dakika ya 9) na Christopher Tibandeke (TRA United vs Mtibwa Sugar dakika ya 8).

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA UDHIBITI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Juni 8, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 189: TRA United 2-1 Mtibwa Sugar

Mchezaji wa Mtibwa Sugar, Magata Fredrick amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwaV faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kurudi uwanjani na kuwa sehemu ya mchezo licha ya kufanyiwa mabadiliko na timu yake.

Magata alifanya tukio hilo Sekunde chache baada ya kufanyiwa mabadiliko na alipoona timu yake ikishambuliwa alirudi uwanjani hivyo kufanya wachezaji wa timu ya Mtibwa kuwa 12. Baada ya shambulio hilo, Magata alitoka nje huku akijificha nyuma ya wachezaji wa timu yake ili asionekane na waamuzi. Kosa hili ni kinyume na kanuni ya17:30 kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Klabu ya TRA United imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Etienne Ndayiragije kutokuhudhuria kwenye mkutano wa waandishi wa habari siku moja kabla ya mchezo bila kutoa taarifa na badala yake alifika kocha msaidizi kinyume na kanuni ya 17:58 kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 191: Coastal Union 12 Simba SC

Mchezaji wa Coastal Union, Meshack Abraham amefungiwa michezo mitatu (3) kwa kosala kumchezea mchezo usio wa kiungwana (rafu) mchezaji wa Simba Anicet Oura nakuhatarisha usalama wake.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5 Udhibiti kwa Mchezaji.

Mechi Namba 193: TRA United 12 Fountain Gate

Klabu ya TRA United imetozwa faini ya Sh. 11,000,000 (milioni kumi na moja) kwa kosala Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Etienne Ndayiragije kutokuhudhuria kwenye mkutano nawaandishi wa habari siku moja kabla ya mchezo bila kutoa taarifa na badala yake kuwakilishwa na Kocha Msaidizi kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:58 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Hili ni kosa la kujirudia kwa Kocha huyo ambapo licha ya klabu hiyo kukumbushwa kuhusu utekelezaji wa kanuni hiyo bado kocha huyo hakuhudhuria mikutano hiyo kwenye michezo mitano (5) mtawalia. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 197:  Simba SC 1-0 Dodoma Jiji FC

Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mtoto muokota mipira kuchukua chupa za maji zilizokuwa pembeni ya goli ya Dodoma Jiji nakumwaga maji yaliyokuwa ndani ya chupa hizo na baadae kuondoka na taulo la mlinda mlango wa Dodoma jiji.

Baada ya mtoto muokota mipira kuondoka na taulo hilo, mlinda mlango huyo na mchezaji Andy Bikoko walimfuata wakimtaka kurejesha taulo hilo, lakini baadhi ya washabiki wa Klabu ya simba waliokua karibu na eneo hilo walianza kurusha chupa zenye vimiminika kwa wachezaji hao wa Dodoma Jiji.

Kitendo hicho cha mtoto muokota mipira kumwaga maji, kuondoka na taulo na washabiki wa Simba kurusha chupa, vinatafsiriwa kutokuwa vya kiungwana.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mshabiki wa klabu ya Simba, Omary Omary (maarufu kwa jina la Bomba) amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12 kwa kosa la kufanya fujo kwenye vyumba vyakubadilishia nguo vya timu ya Dodoma Jiji akimtuhumu kiongozi wa Dodoma Jiji aliyekuwa ndani ya chumba hicho na imani za kishirikina.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 199:  Young Africans 3-1 Namungo FC

Mashabiki wa Young Africans, Baraka Shekimweri (maarufu kwa jina la Baraka Yanga) na Abdulrahman Saidi (maarufu kwa jina la Fumau Mshairi) kwa Pamoja wamefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kwa kosa la kukiuka utaratibu maalumu wa kuketi uwanjani.

Mashabiki hao kwa pamoja wakiwa na tiketi zenye hadhi ya kuketi kwenye jukwaa la VIP B, walilazimisha kwenda kwenye jukwaa lenye hadhi ya VIP A licha ya kuelekezwa na watu wa tiketi kuwa hawana sifa ya kuketi jukwaa hilo, Mashabiki hao waliruka uzio unaotenganisha maeneo hayo na kwenda jukwaa la VIP A kinyume na utaratibu maalumu wa uwanjani hapo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:2 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 206: Mbuni 0-1 TMA 

Klabu ya Mbuni ya Mkoani Arusha imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kutokuheshimu ratiba ya mtiririko wa matukio hivyo kuingia uwanjani kwa kuchelewa kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:33 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo

Mchezaji wa Mbuni, Yunus Lema ametozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kukwepa kupeana mikono na timu mgeni kabla ya mchezo ilihali alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Yunus alielekea kwenye benchi la timu yake wakati ambao timu mgeni na timu mwenyeji walikuwa wakipeana mikono kabla ya mchezo kuanza.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.4) kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji

Mechi Namba 207: African Sports 1-3 Polisi Tanzania

Klabu ya African Sports ya Mkoani Tanga imepewa adhabu ya onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na wawakilishi wanne (4) badala ya wawakilishi wa tano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2(2.1).Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu taratibu za mchezo.

GEITA ‘WANATUPIA’ MABAO TU.

Geita Gold imeendelea kuonyesha ‘ubabe’ wake kwenye Ligi ya Championship ya NBC baada ya kutupia mabao 63 ikiwa ni idadi kubwa hadi sasa msimu wa 2025/2026.

Timu hiyo iliyopo katika mbio za kurejea Ligi Kuu ya NBC baada ya kushuka msimu wa 2023/2024 ikiwa ni takribani misimu miwili ikicheza Ligi ya Championship huku ikiongoza msimamo na alama 68.

Kagera Sugar iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo na Mbeya Kwanza iliyopo nafasi ya tatu nazo haziko nyuma ikiwa zimeweza kutikisa nyavu za wapinzani wake mara 52.

Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro ipo nafasi ya tatu kwa timu zenye mabao mengi ambapo imefunga mabao 47 yanayoiweka katika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Transit Camp haipo mbali ikiwa imetikisa nyavu za wapinzani wao mara 39 huku ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Kwa upande wa ‘wajeda’ wa Mbuni wenye maskani yake mkoani Arusha imefanikiwa kufunga mabao 37 ndani ya Ligi hiyo huku ikiwa nafasi ya sita katika msimamo.

 

CHIRWA AJIPATA CHAMPIONSHIP.

MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar Obrey Chirwa amejipata baada ya kuzidi kutupia mabao  kwa kufikisha 17 hadi sasa ndani ya Ligi ya Championship ya NBC.

Ligi hiyo imeshachezwa mizunguko 28 huku ikiwa imesalia mizunguko miwili ili Ligi hiyo kufikia ukingoni ambapo pia mchezaji huyo ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo huku ikipanda Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 68.

Maulid Shaban wa Geita Gold hayupo mbali akiwa amefanikiwa kuifungia mabao 16 timu yake ambayo ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC na imeshakata tiketi ya kucheza Ligi Kuu baada ya kukusanya alama 71.

Ramadhani Kalanje wa timu ya B19 nae ameweza kutikisa nyavu za wapinzani wao mara 13 huku timu hiyo ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo ikikusanya alama 34.

Abdereheman Mussa wa Transit Camp iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya nne wameweza kufunga mabao 12 kila mmoja.

Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp kabla ya kuhamia KMC ya Ligi Kuu ya NBC, Boniface Brown,Joseph Ambukege wa Mbeya Kwanza na Samson Kassian wa KenGold wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja hadi sasa kwenye ligi hiyo.