Author: Loveness Bernard

KENGOLD ,MASHUJAA HAPATOSHI SOKOINE LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa mzunguko wa 23 kuanza rasmi katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya majira ya saa kumi alasiri.

Timu ya KenGold ndio mwenyeji wa mchezo huo ikiikaribisha timu ya Mashujaa kutoka Kigoma ambapo timu zote mbili zikitaka alama tatu muhimu.

KenGold  iko nafasi ya 16  kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 15 huku wakifunga mabao 18 na kuruhusu mabao 38 .

Mashujaa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 23 kufungaa mabao 17 na kuruhusu mabao 26.

Mchezaji wa kuchungwa katika mchezo huo wa kikosi cha  KenGold  ni Seleman Bwenzi akiwa amecheza michezo sita na kufunga mabao matano ikiwa ni mchezaji aliyeingia kwenye dirisha dogo la usajili.

Kwa upande wa Mahujaa mchezaji wa kuchungwa ni David Ulomi akiwa amefunga mabao manne.

 

AZAM,NAMUNGO WAGAWANA ALAMA,PAMBA KUKIWASHA NA YANGA LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo miwili ya mzunguko wa 22 kuchezwa viwanja viwili jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza ulichezwa saa kumi jioni ambapo timu ya JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya KenGold kutoka Mbeya katika uwanja  wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam.

Mchezo ulianza kwa kasi ambapo kila mchezaji alipambana kuhakikisha  timu yake inapata alama muhimu ,dakika ya 45 mchezaji wa JKT, Edward Songo aliipatia timu yake goli  kwa  mkwaju wa penati  hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili kianza ambapo Ken Gold walionekana wakilisaka kwa kasi lango la JKT Tanzania na dakika ya 85 mchezaji wa wao Selemani Bwenzi aliwaamsha mashabiki wa ‘makarasha’ kwa kuipatia timu yake bao la  kusawazisha  na kufanya mchezo kuisha wakiwa wamegawana alama moja moja.

Mchezaji wa Ken Gold Seleman Bwenzi alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo  baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

JKT Tanzania wamefikisha alama 27 wakiwa wamefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 16 na wakiwa nafasi ya sita baada ya kucheza mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC 2024/2025.

KenGold wanaendelea kusalia nafasi ya 16 kwenye msimamo wakiwa na alama 15 wakifunga mabao 18 kuruhusu 38 baada ya mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa pili ni timu ya Azam iliwapokaribisha timu ya Namungo katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi mchezo uliochezwa saa moja jioni.

Ilimchukua dakika 12 mchezaji wa  Namungo, Hamis Halifa kuwaweka mbele timu yake kabla ya mchezaji wa Azam, Gibril Sillah kuweka mzani sawa  katika dakika ya 43 ya mchezo huo hivyo timu zote kwenda mapumziko ubao ukisomeka  1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa mchezo.

Mlinda mlango wa Namungo, Jonathan Nahimana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Azam wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na alama 45 wakifunga mabao 32 kufungwa 12 huku Namungo wakiwa nafasi ya 12 wakiwa na alama  23 wakifunga mabao 16 na kuruhusu mabao 27.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili ambapo timu ya Pamba Jiji itawakaribisha Young Africans katika uwanja wa CCM Kirumba huku Tabora United wakiwakaribisha Dodoma Jiji katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

JKT,KEN GOLD HAPATOSHI LEO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea kwa michezo miwili inayopigwa mkoani Dar es salaam katika viwanja vya Meja Jenerali Isamuhyo na Azam Complex.

JKT Tanzania wazee wa ‘kichapo cha kizalendo’ itawakaribisha Ken Gold ‘wazee wa makarasha’ katika mchezo utakaochezwa saa kumi alasiri.

Ikumbukwe kuwa JKT Tanzania ipo nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa imefunga mabao 15 ikiruhusu mabao 15 na kukusanya alama 26 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kwa upande wa Ken Gold ipo nafasi 16 ikiwa imefunga mabao 17 ikiruhusu 37  ikiwa imekusanya alama 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa pili utachezwa Azam Complex uliopo Chamazi Dar es Salaam majira ya saa moja usiku ambapo timu ya Azam itawakaribisha Namungo.

Azam ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao 31 ikiruhusu mabao 11 na  ikikusanya alama 44 .

Namungo ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao 15 ikiruhusu mabao 26 na kukusanya alama 22.

 

FOUNTAIN GATE YAJIPATA,MASHUJAA MAMBO MAGUMU

LIGI Kuu ya NBC jana michezo iliendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa mikoa mitatu tofauti Manyara,Singida na Kagera.

Fountain Gate iliwakaribisha timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mchezo uliochezwa majira ya saa nane mchana.

Dakika ya 27  Fountain Gate walipata bao kupitia mchezaji wao Amos Kadikilo kwa mkwaju wa penati na ambalo ndio bao pekee katika mchezo huo na lilipelekea timu hiyo kuvuna alama zote tatu na kufikisha alama 25 nafasi ya nane ya katika msimamo wa Ligi Kuu.

Mchezaji wa Fountain Gate Amos Kadikilo alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo dhidi ya timu ya Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 14 ikiwa na alama 18.

Singida Black Stars iliwaalika Mashujaa majira ya saa kumi alasiri uwanjani CCM Liti, mchezo ulianza kwa kasi na timu zote zilishambuliana kwa kasi hadi kufikia mapumziko hakuna aliyeona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza ambapo dakika ya 57 mshambuliaji wa Singida,Jonathan Sowah alifungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati na dakika ya 60 aliongezea bao la pili huku Elvis Rupia akiongeza bao la tatu dakika ya 90 ya mchezo huo ambao uliisha kwa ubao kusomeka 3-0.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo akiisaidia timu yake kufikisha alama 41 wakiwa nafasi  ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 11 na wakivuna alama 23.

Mchezo wa mwisho ni Kager Sugar iliwakaribisha timu ya KMC majira ya saa moja jioni katika uwanja wa Kaitaba.

Mchezo ulikuwa wa kasi ambapo timu zote mbili zilikuwa zikishambuliana kwa kasi jambo lililopelekea mcheo huo kumalizika kwa 0-0 na mchezaji wa Kagera Sugar,Eric Mwijage atichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.Kagera walifikisha alama 16 wakiwa nafasi ya 15 huku KMC wakiwa nafasi ya 10 na alama 24.

LADHA ZA LIGI KUU KUCHEZWA VIWANJA VITATU

LIGI Kuu ya NBC itaendelea leo kwa mzunguko wa 22  kuanza kuchezwa  katika viwanja vitatu tofauti nchini kuanzia saa nane mchana.

Mchezo wa kwanza utakaochezwa leo saa nane mchana ni timu ya Fountain Gate itaikaribisha timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara majira ya saa nane mchana.

Fountain Gate ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku  ikiwa imevuna alama 22 na kufunga mabao 25 na kufugwa 39 na Tanzania Prisons ipo nafasi ya 14 ikiwa na alama 18 mabao y kufunga 12 na kufungwa 26.

Singida Black Stars itaikaribisha timu ya Mashujaa katika uwanja wa CCM Liti mkoani Singida mchezo utakaochezwa majira ya saa kumi jioni.

Singida Black Stars ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imefunga mabao 28 na kuruhusu nyavu zao kufungwa mara 19, Mashujaa ipo nafasi ya tisa katika msimamo ikiwa imefunga mabao 17 na kufunwa mabao 23.

Mechi ya mwisho leo itachezwa majira ya saa moja jioni ambapo timu ya Kagera Sugar itaikaribisha timu ya KMC katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Kagera Sugar ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo ikiwa imefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 30 huku KMC ikiwa nafasi ya 10 ikiwa na alama 23 na ikifunga mabao 15 na kuruhusu 32.