Author: Loveness Bernard

BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB) KUPOKEA MABORESHO YA KANUNI ZA LIGI

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inautaarifu umma kuwa imeanza kupokea maoni ya maboresho ya Kanuni za Ligi kwa toleo la mwaka 2026. Maoni/mapendekezo hayo ya maboresho ya kanuni ni kwa ajili ya Ligi Kuu Ligi ya Championship na First League.

Lengo la zoezi hili ni kuboresha Kanuni za Ligi ili ziweze kutatua changamoto zilizojitokeza na zinazoweza kujitokeza katika msimu wa 2025/2026. Mchakato huu wa kupokea maoni utafanyika kwa kipindi cha majuma manne (4) na umefunguliwa rasmi Aprili 22, 2026.

Bodi inawakumbusha wadau wote kuwa kanuni bora ni msingi wa kuwa na ligi bora na maendeleo ya mpira wa miguu kwa ujumla, hivyo ushiriki wa kila mdau ni jambo la muhimusana.

Maoni ya maboresho ya kanuni yawasilishwe TPLB kabla ya Mei 22, 2026 kwa kupitia njia zifuatazo;

i. Barua pepe – maoni@ligikuu.co.tz

ii. Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) au WhatsApp +255 758 500 222

iii. Kuwasilisha kwa mkono katika ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania zilizopo

ghorofa ya 14 kwenye jengo la NSSF (Mafao House), Ilala – Dar es Salaam.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Aprili 18, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 07: TRA United FC 0-0 Simba SC

Klabu za TRA United na Simba za Dar es Salaam zimetozwa faini Sh. 5,000,000 (milioni tano) kila moja kwa kosa la walinzi wa klabu hizo (Stewards) kupigana mara baada ya timu hizo kuwasili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 132: Pamba Jiji FC 0-3 Young Africans SC

Mchezaji Mudathir Yahya wa klabu ya Young Africans amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham wakati mchezo unaendelea kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 146: Coastal Union FC 1-1 Mtibwa Sugar FC

Klabu ya Coastal Union ya mkoani Tanga imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa za maji kiwanjani wakati mwamuzi wa kati na mwamuzi msaidizi namba moja wakiwa wanatuliza vurugu zilizokuwa zikiendelea baada ya mchezaji wa Mtibwa Sugar, Victor Collins kumsukuma mchezaji wa Coastal Union Athuman Makambo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Mechi Namba 151:  TRA United 2-0 Singida BS

Klabu ya Singida BS ya mkoani Singida imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la viongozi wake wawili kuingia kiwanjani na kumwaga vimiminika. Viongozi hao walifanya tukio hilo lililotafsiriwa kama vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina, kabla ya timu kutoka kwa ajili ya kupasha moto misuli. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 152: Azam FC 0-0 Simba SC

Klabu ya Azam ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la viongozi wa benchi la ufundi pamoja na wachezaji kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo na makubaliano yaliyofanyika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo huo. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo huo, mara baada kunyoosha kibendera kuashiria mchezaji wa Simba kuotea.

Hili ni kosa la kujirudia kwa klabu ya Simba ambapo ndani ya msimu huu wa Ligi kuu ya NBC 2025/2026, mashabiki wa klabu hiyo walitenda kosa hilo katika michezo miwili tofauti na kusababisha klabu kuadhibiwa. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

MASHUJAA, SINGIDA ‘KUKINUKISHA’, YOUNG AFRICANS, MBEYA CITY VITA YA ALAMA TATU LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo katika mikoa ya Kigoma na Dar es Salaam ambapo timu ya Mashujaa itaikaribisha timu ya Singida Black Stars katika uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma huku Young Africa ikiikabili Mbeya City katika uwanja wa KMC Complex, Dar.

Mchezo wa kwanza utaanza majira ya saa 10:00 alasiri kwa Mashujaa kuikaribisha timu ya Singida Black Stars mchezo huo ukiwa ni muhimu kwa timu hizo ili kufikia malengo waliyojiwekea ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC.

Mashujaa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 18 ikishinda michezo minne, sare nane na kufungwa michezo sita huku ikifanikiwa kukusanya alama 20.

Wachezaji wa Singida

Singida ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 18 kushinda michezo 8 sare nne na kufungwa michezo sita huku ikikukusanya alama 28.

Kwa upande wa mchezo wa Young Africans na Mbeya City utachezwa majira ya saa 12:30 jioni ikiwa ni mchezo utakaokuwa na upinzani mkali baada ya timu hizo kutoka sare kwenye mchezo wao wa mzunguko wa kwanza.

Wachezaji wa timu ya Young Africans.

Young Africans ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 18 ushindi 13 na sare tano ikiwa ni moja ya timu ambazo hazijapoteza mchezo wowote sawa na Azam huku ikiweza kukusanya alama 44.

Wachezaji wa Mbeya City.

Mbeya City ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 18, ikishinda michezo minne, sare tano na kufungwa michezo tisa huku ikiweza kukusanya alama 17.

FOUNTAIN, SIMBA ‘KUKIPIGA’ COASTAL KUIKARIBISHA DODOMA JIJI LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo katika mikoa ya Arusha na Tanga ambapo timu ya Fountain Gate itaikaribisha timu ya Simba katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku Coastal ikiikabili Dodoma Jiji katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Mchezo wa kwanza utaanza majira ya saa 10:00 jioni kwa Fountain Gate kuikaribisha timu ya Simba, mchezo huo ukiwa muhimu kwa timu hizo ikiwa ni moja ya kufikia malengo waliyojiwekea.

Fountain Gate iko nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 17 ikishinda michezo minne, sare nne na kufungwa michezo tisa huku ikifanikiwa kukusanya alama 16.

Wachezaji wa Simba.

Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 17 kushinda michezo 10 sare sita na kufungwa mchezo mmoja huku ikiweza kukusanya alama 36.

 

Kwa upande wa mchezo wa Coastal Union utapigwa majira ya saa kumi na mbili jioni ikiwa ni mchezo wa kimbinu kwani kila timu ikizitaka alama zote tatu muhimu ili kusonga mbele ndani ya malengo waliyojiwekea msimu huu.

Coastal Union iko nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 18 ushindi tatu, sare saba na kufungwa michezo nane huku ikiweza kukusanya alama 16.

Wachezaji wa Dodoma Jiji.

Dodoma Jiji ipo nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 18 ikiwa imeshinda michezo sita, sare sita na kufungwa michezo sita huku ikiwa imekusanya jumla ya alama 24.

KMC, PRISONS NANI KUMFUNGA PAKA KENGELE LIGI KUU YA NBC?

LIGI Kuu ya NBC inarejea rasmi leo mkoani Dar es Salaam kwa mchezo mmoja baada ya mapumziko mafupi kwa ajili ya michezo ya Kombe la Shirikisho ambapo timu ya KMC itaikaribisha timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa KMC Complex majira ya saa 1:00 usiku.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili kwani zinatafuta nafasi ya kubaki katika Ligi Kuu ya NBC kutokana na kuwa nafasi mbaya katika msimamo.

KMC iko nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 18 kwa kushinda michezo miwili, sare mbili na kufungwa michezo 14 huku ikiwa imekusanya alama nane tu.

Prisons ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 18 kwa kushinda michezo mitatu, sare nne na kupoteza michezo 11 huku ikiwa imekusanya jumla ya alama 13.