Author: Loveness Bernard

OKELLO,GONCALVES WANG’ARA TUZO ZA TFF APRIL

Kiungo mshambuliaji wa Young Africans, ALLAN OKELLO, amechaguliwa kuwa MchezajiBora wa mwezi Aprili wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku PEDRO GONCALVES wa Young Africans, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Okello alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Pacome Zouzoua waYanga na Idd Selemani wa Azam FC, alioingia nao fainali katika mchakato wa tuzo zamwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu aliyochezamwezi huo, akifunga bao moja na kuhusika na mengine sita kwa dakika 320 alizocheza.

Kwa upande wa Pedro aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Etiene Ndairagijewa TRA United, aliiongoza Young Africans kushinda michezo yote mitatu iliyochezamwezi huo na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, ikifunga mabao 12 nahaikuruhusu bao. Young Africans ilizifunga Tanzania Prisons (3-0), Mbeya City (6-0) naPamba Jiji (0-3).

Wakati huohuo Kamati ya Tuzo, imemchagua HASSAN MWATEREMA wa Kagera Sugar kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Aprili wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/26, hukuJUMA KASEJA pia wa Kagera Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Mwaterema aliyeingia fainali na Japhet Mayungu wa TMA na Salum Mlemwa wa Gunners, alionesha kiwango chenye mwendelezo, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili kwadakika 139 za michezo miwili aliyocheza.

Kwa upande wa Kaseja aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Geita Gold na MbwanaMakata wa Polisi Tanzania, aliiongoza timu yake kushinda michezo yote miwili iliyochezamwezi huo ikiendelea kubaki nafasi ya pili.

Pia Kamati ya Tuzo imeteua MAGOLI MATATU BORA ambayo yatapigiwa kura namashabiki ili kupata goli bora la mwezi la mashabiki. Magoli hayo ni Pacome Zouzoua(Young Africans vs Mbeya City dakika ya 43), Idd Kipagwile (Dodoma vs Fountain Gate dakika ya 68) na Grayson Gwalala (Coastal v Dodoma Jiji dakika ya 14).

FEISAL HAKAMATIKI PASI ZA MABAO LIGI KUU YA NBC.

VITA ya pasi za mabao imezidi kushika kasi kutokana na namna wachezaji mbalimbali wanavyopambana kuhakikisha wanazidi kusaidia timu zao kupata alama za Ligi Kuu ya NBC.

Kiungo wa Azam Feisal Salum ndio kinara wa pasi za mwisho akiwa amecheza michezo 21 ya Ligi Kuu ya NBC, ndani ya dakika 1721 ameweza kutoa pasi za mabao nane.

Elie Mpanzu nae hayuko mbali amefanikiwa kucheza dakika 842 ndani ya michezo 17 ya Ligi Kuu ya NBC akitoa pasi za mabao saba mpaka sasa.

Allan Okello wa Young Africans ambaye aliingia dirisha dogo la usajili amecheza micheza 16 ambayo ni sawa na dakika 1128 amefanikiwa kutoa pasi za mabao saba.

Duke Abuya wa Young Africans anashika nafasi ya nne akiwa amecheza michezo 21 ya Ligi Kuu ya NBC sawa na dakika 1736 zilizomwezesha kutoa pasi za mabao tano.

Kwa upande wa Lamin Jarjou anaeichezea Singida Black Stars amecheza michezo 19 ikiwa sawa na dakika 1231 na kutoa pasi za mabao tano ndani ya Ligi Kuu ya NBC.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

TAARIFA YA KAMATI YA USIMAMIZI WA LIGI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB).

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Mei 9, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 169: Simba SC 2-2 Young Africans

Klabu ya Young Africans imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Saalam kuelekea mchezo tajwa hapo juu Mei3, 2026. Young Africans iliwasili uwanjani saa 10:35 alasiri badala ya saa 10:30 alasiri jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Young Africans imetozwa faini ya Sh. 30,000,000 (milioni thelathini) kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja upande wa pili wa Barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.

Meneja wa Klabu ya Young Africans Walter Harson amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Simba Clatous Chama kwenye mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha na Maofisa Wengine wa Ufundi.

Shabiki wa klabu ya Young Africans aliyetambulika kwa jina la Mohamed Ally Mposo ambae amekuwa akiambatana na maofisa wa ufundi wa klabu hiyo amefungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi 12 kwa kosa la kuingia kwenye eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kumwaga vimiminika kitendo kilichotafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 Mechi Namba 154: Mtibwa Sugar 0-1 Dodoma Jiji FC

Klabu ya Dodoma Jiji ya Dodoma imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) huku wakiwa pungufu bila kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kikanuni, Dodoma Jiji iliwakilishwa na wawakilishi wawili pekee badala ya watano huku wakiwa hawana vifaa kamili kinyume na matakwa ya kanuni 17:2 (2.2).

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 172: Geita Gold 6-1 Hausung FC

Klabu ya Hausung ya Mkoani Njombe imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la maofisa wake kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika 20, maofisa hao walifika saa 1:35 usiku badala ya saa 1:15 usiku kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2 (2.2) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo

Mechi Namba 182: TMA FC 2-0 Gunners FC

Mchezaji wa TMA Said Kulwa amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuonekana na chupa yenye kimiminika na kumwaga kimiminika hicho kwenye upande wa timu ngeni wakati wa ukaguzi wa uwanja jambo lililotafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwaWachezaji.

Wachezaji Mohamed Lipangala na Joel Stephano wa TMA FC, wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja kwa kosa la kuonekana wakichimbia vitu kwenye nguzo ya timu yao jambo lililo tafsiriwa kama imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mechi Namba 190: Mbeya Kwanza vs Hausung FC

Klabu ya Hausung FC ya mkoani Njombe imepoteza mchezo tajwa hapo juu na Timu ya Mbeya Kwanza ya mkoani Tabora imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama (3) kwa kosa la Hausung FC kushindwa kufika kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora bila sababu za msingi na zinazokubalika hivyo kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.

Sambamba na adhabu hiyo, Hausung FC imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi)na kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo Pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa Ligi ya Championship.Pia Mwenyekiti wa klabu ya Hausung FC, Erasto Haule amefungiwa kwa kipindi cha mwakammoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani.

Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1(1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship kuhusu Kutofika Uwanjani.

First League

Mechi Namba 37B: Alliance FC 0-3 IAA FC

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la maofisa wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwakosa la shabiki wake kumvamia mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Julius Ottu na kumpiga ngumi usoni.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi Namba 41A: Nyumbu FC 1-1 Moro Kids

Timu ya Moro Kids ya Mkoani Morogoro imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye uwanja wa mchezo Filbert Bayi Mkoani Pwani. Moro Kids ilifika saa 8:35 badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 43A: Magnet FC 0-2 Bandari Tanzania

Klabu ya Magnet ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la maofisa wake kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi yamchezo (MCM) kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Maofisa hao ilipofika muda wa kikao waligoma kushiriki kikao hicho kwa madai wanamsubiri mwenye timu afike ndipo washiriki kikao hicho, hata alipofika kiongozi huyo (Tuntufye Mwambusi) bado maofisa hao hawakushiriki kikao hicho kwa madai ya kutojibiwa barua yao waliyoiwasilisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 46A: Green Warriors 1-5 Magnet

Timu ya Magnet ya Mkoani Dar es Salaam imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye uwanja wa mchezo Filbert Bayi Mkoani Pwani. Magnet ilifika saa 8:35 badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

 

NYASI ZA MIKOA MITATU ‘KUWAKA MOTO’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inarejea leo baada ya mapumziko ya takribani siku 10 ambapo mzunguko wa 22 utaanza leo katika mikoa ya Arusha, Mbeya na Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza utakuwa mkoani Arusha ambapo Fountain Gate itaikaribisha timu ya Pamba Jiji katika uwanja wa Sheikhe Amri Kaluta majira ya saa 8:00 mchana.

Fountain Gate inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo 19 ushindi mitano, sare nne na kupoteza michezo 10 huku ikikusanya jumla ya alama 19.

Pamba Jiji ipo nafasi ya saba ikiwa imeshinda michezo sita, sare nane na kufungwa michezo mitano ndani ya michezo 19 ambayo timu hiyo imecheza huku ikikusanya alama 26.

Mchezo wa pili utakuwa majira ya saa kumi na robo ambapo Mbeya City itaikaribisha timu ya Mashujaa katika uwanja wa Sokoine.

Mbeya City ipo nafasi ya 14 Kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza michezo 19 kushinda michezo minne, sare tano na kufungwa michezo 10 huku ikiweka kibindoni alama 17.

Mashujaa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza michezo 19 ushindi nne, sare tisa na kufungwa michezo sita huku ikikusanya alama 21.

Mchezo wa mwisho utakuwa majira ya saa kumi na mbili jioni ambapo timu ya JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa KMC katika uwanja wa KMC Complex.

JKT Tanzania ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza michezo 19, ushindi saba,sare nane na kupoteza michezo minne .

KMC ipo nafasi ya 16 ikiwa imecheza michezo 19 ushindi miwili, sare tatu na kufungwa michezo 14.

KARIAKOO DABI KUPIGWA MEJA JENERALI ISAMUHYO.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inatangaza mabadiliko ya uwanja wa mchezo namba 169 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026, kati ya klabu ya Simba na klabu ya Young Africans, maarufu kama ‘Kariakoo Derby’.

Mchezo huo ambao hapo awali ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, sasa utachezwa kwenye uwanja wa Mej. Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam Mei 3, 2026 kuanzia saa 12:00 jioni.

Sababu ya mabadiliko hayo ni uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa kwenye matengenezo.

Klabu za Simba na Yanga pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu ya NBC wamepatiwa taarifa zote kuhusiana na mabadiliko ya uwanja wa mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na hadhi ya michezo mikubwa ya Ligi ya sita kwa ubora barani Afrika.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inawatakia maandalizi mema wadau wote wa mchezo.