Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 032: Singida BS FC 1-3 TRA United FC
Mchezaji Khalid Aucho wa klabu ya Singida BS ya mkoani Singida amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mchezaji Adam Adam wa klabu ya TRA United wakati wa mchezo tajwa hapo juu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Alex Pancras kutoka Dar es Salaam amepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Khalid Aucho.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mechi Namba 031: Simba SC 0-2 Azam FC
Mchezaji Jonathan Sowah wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga kiwiko mchezaji Himid Mao wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mchezaji Allasane Kante wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga teke kwa makusudi mchezaji Feisal Salum wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji Jonathan Sowah na Allasane Kante katika mchezo huo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mechi Namba 046: Coastal Union FC 0-1 Young Africans SC
Klabu ya Young Africans ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
MUHIMU
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake. Ukumbusho huu unakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.
Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa Ligi yetu jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani.
Ligi ya Championship ya NBC
Mechi Namba 061: African Sports Club 0-2 Transit Camp FC
Klabu ya Transit Camp ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne (4) badala ya watano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.1) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
First League
Mechi Namba 7A: Alliance FC vs Biashara United
Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na pointi tatu (3) katika mchezo tajwa hapo juu, huku Biashara United ikipoteza mchezo huo kwa mujibu wa Kanuni ya 17:31 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.
Biashara United ilisababisha mchezo huo kuvunjwa katika dakika ya 67 baada ya wachezaji wawili (2) wa timu hiyo iliyoanza mchezo ikiwa na wachezaji wanane (8) tu, kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo hivyo kufanya timu hiyo kusalia na wacheza sita (6) pekee ambao hawawezi kufanya mchezo uendelee kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:30 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 10A: Pan African FC vs Moro Kids FC
Klabu ya Pan African ya mkoani Dar es Salaam imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya Moro Kids imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Pan African kushindwa kuandaa mchezo huo kikamilifu, jambo lililosababisha mchezo huo kushindwa kufanyika kwa mujibu wa Kanuni.
Pan African ilishindwa kupeleka uwanjani gari maalum la kubebea wagonjwa (Ambulance) kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo, hata baada ya kupita dakika 30 za kusubiri kwa mujibu wa kanuni.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo na Kanuni ya 32:1 ya First League kuhusu Kuvuruga Mchezo.

