Ladha za NBC Championship zinaendelea Leo, Februari 22, 2025, ambapo pazia la mzunguko wa 19 wa Ligi hiyo linafunguliwa rasmi kwa michezo saba itakayochezwa katika mikoa saba tofauti nchini. Kuanzia saa 10:00 alasiri, kila timu ikisaka alama tatu zenye uzito wa dhahabu katika safari ya kutimiza malengo yake.
Mbeya Kwanza vs Transit Camp
Mchezo unaovuta hisia zaidi ni kati ya Mbeya Kwanza na Transit Camp utakaopigwa katika Uwanja wa Airtel, mkoani Singida. Mbeya kwanza inatumia uwanja huo kama uwanja wake wa nyumbani kufuatia kufungiwa kwa Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.
Mbeya Kwanza inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 40, huku Transit Camp ikifuatia katika nafasi ya nne na alama 36, Ushindi kwa Mbeya Kwanza utaifanya kufikisha alama 43 na kuimarisha nafasi yao katika mbio za kupanda Ligi Kuu ya NBC. Kwa Transit Camp, ushindi utaifanya kufikisha alama 39 na kupunguza kwa kiasi kikubwa pengo dhidi ya wapinzani wao wa moja kwa moja.
Mchezo huo utarushwa mubashara kupitia jukwaa la FIFA+ ukitoa fursa kwa mashabiki kote nchini kushuhudia patashika hiyo.
Vinara Kwenye Jaribio Zito
Geita Gold, vinara wa ligi hadi sasa na timu pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu, watakuwa ugenini Moshi kuivaa Polisi Tanzania katika Uwanja wa Ushirika. Rekodi yao safi iko hatarini kila wanaposhuka dimbani, na kila mpinzani anatamani kuwa wa kwanza kuwavua ubabe huo. Je Polisi Tanzania watafanikiwa kuivunja rekodi hii ?
Michezo Mingine
Michezo mingine ya mzunguko huu ni:
- TMA dhidi ya KenGold katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
- Stand United dhidi ya Hausung katika Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
- BigMan dhidi ya Barberian katika Uwanja wa Ilulu, Lindi.
- B19 wakiwakaribisha Gunners katika Uwanja wa TFF Center, Kigamboni.
- African Sports dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo utakaokamilisha ratiba ya leo.
Kwa ujumla, mzunguko huu wa 20 unatarajiwa kuongeza ushindani na kuathiri kwa kiasi kikubwa mwenendo wa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC kadri mbio za kupanda daraja zinavyozidi kushika kasi.