Author: Yahaya Abushehe

KILUVYA

KILUVYA YASALIA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

TIMU ya Kiluvya ya Mkoani Pwani imefanikiwa kubakia kwenye Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu unaofuata baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Transit Camp hivyo kufanikiwa kubaki kwa ushindi wa jumla (aggregate) wa mabao 4-3.

 

 

Mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa TFF Technical Center – Kigamboni Transit Camp iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

 

Kiluvya iliyopanda daraja kutoka ligi ya First League haikuwa na msimu bora baada ya kumaliza ligi ikiwa imefunga mabao machache (19) sawa na timu ya Cosmopolitan iliyoshuka daraja.

Transit Camp sasa itacheza na Rhino Rangers ya mkoani Tabora kuwania kubakia kwenye Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu ujao wa 2025/2026.

 

Rhino imepata nafasi ya kucheza mchezo huo baada ya kuitoa timu ya Nyumbu kwa tofauti ya mabao 5-3 na itafanikiwa kupanda ligi ya Championship ya NBC ikiwa itaifunga timu ya Transit Camp kwa tofauti kubwa ya mabao kwenye mchezo wa nyumbani na ugenini.

FIRST LEAGUE KUHITIMISHWA LEO.

NBC CHAMPIONSHIP KUHITIMISHWA LEO.

PAZIA la Ligi ya Championship ya NBC linafungwa leo Mei 11 kwa michezo nane kupigwa kwenye viwanja nane tofauti kuanzia saa 10:00 alasiri.

Michezo ya Leo itamtambulisha bingwa wa Ligi ya Championship ya NBC Kati ya Mtibwa Sugar au Mbeya City pia kujua ni timu gani itaungana na Biashara United kushuka daraja.

Mtibwa ili kuwa bingwa inahitaji alama moja pekee ili kufikisha alama 69 ambazo haziwezi kufikiwa na Mbeya City na endapo Mbeya City itapata matokeo yoyote tofauti na ushindi Mtibwa itakuwa bingwa.

Kwa upande wa Mbeya City inahitaji kushinda ili kufikisha alama 68 na endapo Mtibwa ikipoteza mchezo wa leo timu hizo zitalingana alama na Mbeya City atakuwa bingwa kwa tofauti ya mabao.

Vita nyengine ni ya kushuka daraja ambapo klabu za African Sports, Cosmopolitan na Transit Camp zipo kwenye hatari ya kushuka na kuungana na Biashara United.

African Sports ina alama 19 wakati Cosmopolitan ina alama 20 na Transit Camp ikiwa na alama 21, michezo ya mwisho hii Leo itatoa hatma ya timu hizo msimu huu

CARGO, KAJUNA ZATAMBA NYUMBANI MTOANO FIRST LEAGUE.

Michezo ya mtoano (PlayOff) kubaki au kupanda ligi ya First League imechezwa Jana Mei 8 ikishuhudiwa timu zilizokuwa nyumbani Cargo ya Dar na Kajuna ya Kigoma zikiibuka na ushindi.

Mchezo wa kwanza katika uwanja wa TFF Center – Kigamboni uliishuhudia Cargo ikiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Tunduru Korosho.

Mchezo wa pili mkoani Kigoma uliishuhudia Kajuna ikiifunga Copco ya Mwanza kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika.

Michezo ya marudiano itapigwa Mei 12 ambapo Tunduru Korosho itaialika Cargo kwenye uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma huku Copco ikiialika Kajuna kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

NI VITA YA KUBAKI NA KUPANDA FIRST LEAGUE LEO.

Michezo ya mtoano (PlayOff) ya kubaki na kupanda First League inachezwa leo Mei 8 ikikutanisha timu mbili kutoka First League ambazo ni Tunduru Korosho ya Ruvuma na Copco ya Mwanza pamoja na timu mbili kutoka kwenye Fainali za mabingwa wa mikoa ambazo ni Cargo ya Dar es Salaam na Kajuna ya Kigoma.

Mechi ya kwanza itakutanisha timu ya Cargo dhidi ya Tunduru Korosho saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa TFF Center Kigamboni uliopo Dar.

Mechi ya pili itakutanisha timu ya Kajuna dhidi ya Copco kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma huku mchezo huo ukitarajiwa kupigwa saa 10:00 alasiri.

Ikumbukwe timu mbili kutoka First league ni zile zilizopoteza michezo ya Mtoano wa kushuka daraja (Relegation Playoffs) na kupata nafasi ya kupambania kubakia kwenye Ligi hiyo kwa msimu ujao.

Timu mbili kutoka Fainali za mabingwa wa mikoa ni zile zilizotolewa kwenye Nusu Fainali na kushika nafasi ya tatu na ya nne kwenye fainali hizo.

RAIS KARIA

RAIS KARIA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA VIENNA, AISHUKURU FIFA.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ametoa shukrani kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa washiriki wa Warsha ya kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu duniani inayohusisha Nchi Wanachama wa UEFA na CAF inayoendelea Vienna, Austria.

Rais Karia amesema ni heshima kwake na shirikisho kushiriki pamoja na mashirikisho mengine kutoka Afrika na Ulaya.

“Ni furaha kuwa miongoni mwa washiriki kwasababu mijadala mingi inasaidia sana na inatupa data za kuweza kuendeleza mpira wa miguu Nchini kwetu”

Amesema kuna haja ya warsha za aina hiyo kuendelea kutolewa zaidi ili kupata maarifa yanayoweza kusaidia katika shughuli za kila siku katika maendeleo ya mpira wa miguu.

Nchi zinazohudhuria kwenye Warsha hiyo ni Finland, Moldova, Wales, Austria, Georgia kutoka UEFA na Gabon, Morocco, Senegal, Tanzania na Cameroon kutoka CAF.