Author: Yahaya Abushehe

NI VITA YA UBINGWA ‘DERBY’ YA KARIAKOO LEO.

 

‘DERBY YA MAAMUZI’ ndivyo unavyoweza kuuita mchezo wa watani wa Jadi ‘Kariakoo Derby’ ndani ya Ligi Kuu ya NBC unachezwa leo saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.

Huu ni mchezo wa kufunga Pazia la Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/2025 lakini pia ndio mchezo utakaotoa Bingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025.

Young Africans inahitaji alama moja pekee ili kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu kwa kuwa itafikisha alama 80 ambazo haziwezi fikiwa na timu nyengine yoyote.

Matokeo ya Ushindi ndio silaha pekee kwa Simba ili kuweza kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025, hii ni kutokana na utofauti wa alama Kati yake na timu inayoongoza Ligi Young Africans.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliopita huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 79.

Mwamuzi wa kati kwenye mchezo huu ni Amin Mohammed Amin, mwamuzi msaidizi namba moja ni Mahmoud Ahmed Abo, mwamuzi msaidizi namba mbili Samil Gamal Saad na mwamuzi wa akiba ni Ahmed Mahrous Elghandour wote kutoka Misri.

KARIAKOO DERBY

KARIAKOO ‘DERBY’ KUPIGWA JUNI 25.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeusogeza mbele mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya klabu ya Yanga na klabu ya Simba ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 15, 2025 kuanzia saa 11:00 jioni.

Mchezo huo sasa utafanyika Juni 25, 2025 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Bodi inazitakia maandalizi mema klabu za Yanga na Simba kuelekea mchezo huo.

HATMA YA GEITA, STAND KUJULIKANA LEO .

HATMA ya kucheza mchezo wa mtoano kushiriki Ligi Kuu ya NBC kujulikana leo ambapo timu ya Stand United itakuwa mwenyeji wa Geita Gold kwenye uwanja wa CCM kambarage, Shinyanga saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Nyankumbu ulimalizika kwa Sare ya mabao 2-2 hivyo kuufanya mchezo wa leo kuwa mgumu zaidi timu zote zikitafuta nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya NBC.

Ushindi, suluhu au sare ya bao 1-1 unaipa nafasi Stand United kusonga mbele kwenye mchezo wa mtoano unaofuata kwa Faida ya mabao ya ugenini.

Ushindi au sare ya mabao 3-3 na kuendelea unaipa Geita Gold nafasi ya kuendelea kwenye mchezo wa mtoano unaofuata kwa faida ya mabao mengi ya ugenini.

Mshindi wa jumla wa michezo hii ya mtoano wa kupanda (Promotions Playoffs) atacheza na timu iliyofungwa kwenye mchezo wa mtoano utakaozikutaisha timu iliyoshika nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu ya NBC.

SIMBA, SINGIDA BS KINAPIGWA LIGI KUU NBC LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Mei 28 kwa mchezo mmoja wa kukamilisha mzunguko wa 28 Kati ya Simba na Singida Black Stars katika uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa mwisho timu hizo kukutana mkoani Singida timu ya Singida ilikubali kichapo cha bao 0-1 mbele ya Simba kwenye uwanja wake wa Nyumbani CCM Liti bao likifungwa na Fabrice Ngoma.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 69 ikishinda michezo 22 ikitoka sare michezo mitatu na kupoteza mchezo mmoja pekee.

Singida Black Stars ipo nafasi ya 4 kwenye msimamo ikiwa na alama 53 baada ya kushinda michezo 16 ikitoka sare mitano na kupoteza michezo sita.

KILUVYA

KILUVYA YASALIA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

TIMU ya Kiluvya ya Mkoani Pwani imefanikiwa kubakia kwenye Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu unaofuata baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Transit Camp hivyo kufanikiwa kubaki kwa ushindi wa jumla (aggregate) wa mabao 4-3.

 

 

Mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa TFF Technical Center – Kigamboni Transit Camp iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

 

Kiluvya iliyopanda daraja kutoka ligi ya First League haikuwa na msimu bora baada ya kumaliza ligi ikiwa imefunga mabao machache (19) sawa na timu ya Cosmopolitan iliyoshuka daraja.

Transit Camp sasa itacheza na Rhino Rangers ya mkoani Tabora kuwania kubakia kwenye Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu ujao wa 2025/2026.

 

Rhino imepata nafasi ya kucheza mchezo huo baada ya kuitoa timu ya Nyumbu kwa tofauti ya mabao 5-3 na itafanikiwa kupanda ligi ya Championship ya NBC ikiwa itaifunga timu ya Transit Camp kwa tofauti kubwa ya mabao kwenye mchezo wa nyumbani na ugenini.

FIRST LEAGUE KUHITIMISHWA LEO.