TIMU ya Azam kutoka Dar es Salaam imeishushia kipigo kizito Dodoma Jiji cha mabao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar.
Hiki ni kipigo kikubwa zaidi hadi sasa kwenye mzunguko wa 28 ukisalia mchezo mmoja pekee utakaopigwa leo kukamilisha mzunguko huo.
Nahodha wa Azam Lusajo Mwaikenda alikuwa mfano wa kuigwa na wenzake baada ya kufungua ukurasa wa mabao kwa timu yake dakika ya sita ya mchezo huku Abdul Sopo, Gibril Sillah, Nassor Saadun na Frank Tiesse wakifunga bao moja kila mmoja na kukamilisha karama hiyo ya mabao.
Dodoma Jiji imepoteza mchezo wa 12 ikisalia nafasi ya saba baada ya kukusanya alama 34 ikiwa imeshinda michezo tisa hadi sasa huku ikihitaji alama tatu pekee kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.
Baada ya kufunga mabao matano Azam imefikisha jumla ya mabao 48 na kushika nafasi ya tatu kwa idadi kubwa ya mabao nyuma ya Simba yenye mabao 62 na Young Africans inayoongoza ikiwa na mabao 71.
 
					