LIGI kuu ya NBC imeendelea kwa timu ya Azam kuwakaribisha TRA United katika dimba la Azam Complex kwenye pambano lililokuwa na ushindani mkubwa na Azam ikiibuka mbabe kwa kushinda mabao 2-0.
Azam wakicheza nyumbani walianza mchezo kwa kasi wakitawala umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi zilizozaa matunda baada ya Jean Ngite kufunga bao la kuongoza dakika ya 28.
Kipindi cha pili dakika ya 70 Iddi Nado aliongeza bao la pili na kuwaamsha mashabiki wa Azam waliofurahia timu yao kuongeza bao na kumaliza na ushindi hivyo kusogea hadi nafasi ya tano ikifikisha alama 16.
Kwa matokeo hayo timu ya TRA United inashika nafasi ya 9 ikiwa na alama 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku mchezo unaofuata itakuwa mgeni wa timu ya Coastal Union iliyopata sare katika mchezo uliopita nyumbani dhidi ya KMC inayoshika mkia kwenye msimamo.

