MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC Mzizima ‘Derby’ kati ya Azam FC na Simba SC unapigwa leo Septemba 26 saa 2:30 usiku New Amaan Complex hapa Visiwani Zanzibar.
Azam FC inaingia kwenye mchezo huu ikiwa tayari imecheza michezo minne ya Ligi Kuu ya NBC ikishinda miwili na kupata sare michezo miwili, huku ikifunga mabao matano na haijaruhusu bao kwenye michezo hiyo minne.
Kwa upande wa Simba SC imecheza michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC na kushinda michezo yote ikiwa na mabao Saba ya Kufunga na kutoruhusu bao.
Mchezo wa mwisho kukutana kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ulioisha Azam FC ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani Benjamin Mkapa ilikubali kichapo cha mabao 3-0, Je Azam kulipa kisasi au Simba kuendeleza ubabe ? Majibu yatapatikana baada ya dakika tisini kumalizika.
Hii ni kwa mara ya kwanza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kuja kuchezwa visiwani Zanzibar, hii ni baada ya maboresho ya kanuni ya msimu 2024/2025.
Kanuni ya 6(4) Michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaweza kuchezwa kwenye viwanja vilivyopo Tanzania Visiwani (Zanzibar) kwa mazingatio ya kanuni ya 9 kuhusu uwanja.