Category: STORY

KMC YASALIA LIGI KUU

TIMU ya KMC ya Dar es Salaam imejihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu NBC msimu 2023/24 baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0.

Ushindi wa mabao 2-1 walioupata Mbeya City katika mchezo wa awali jijini Mbeya, haukutosha kuwahakikishia mapema Wagonga Nyundo hao nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya NBC 2023/24 baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 3-2.

Mabao ya Daruweshi Saliboko na Awesu Awesu yalitosha kuwafanya vijana hao wa Kinondoni kumaliza msimu wakiwa na uhakika wa kushiriki Ligi hiyo msimu ujao.

Kipigo hicho kinaifanya timu ya Mbeya City kusafiri mpaka Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika tarehe 19 Juni kabla ya kurudiana tarehe 24 Juni kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mshindi wa matokeo ya jumla kwenye michezo hiyo ndiye atapata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu NBC msimu wa 2023/24 na atakayefungwa atashiriki Ligi ya Championship kwa msimu ujao.

WABABE WA MABAO LIGI KUU 2022/23

IKITAMATIKA siku sita zilizopita Ligi Kuu ya NBC imeshuhudia jumla ya mabao 561 yakifungwa kwa timu zote 16 zilizoshiriki Ligi hiyo.

Timu ya Simba imeibuka kinara ikifunga jumla ya mabao 75 ikiizidi kwa mabao 14 timu ya Yanga inayoshika nafasi ya pili baada ya kufunga jumla ya mabao 61.

Ikiwa timu ya kwanza kufunga bao katika mashindano ya msimu huu uliomalizika kupitia kwa Ally Bilali Ruvu Shooting imefunga mabao 19 pekee ikiwa ni idadi ndogo zaidi.

Timu ya Polisi Tanzania ya Kilimanjaro itakayoshiriki Ligi ya Championship msimu ujao baada ya kushuka daraja na kuungana na Ruvu imefungwa mabao mengi (54) huku timu ya Simba ikimaliza msimu kwa kufungwa mabao machache (17).

YANGA YAONGEZA NAMBA KATIKA HISTORIA

TIMU ya Yanga imekabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa mara ya 29 ikiwa ni mara saba zaidi ya timu inayofuatia ya Simba iliyotwaa mara 22 na mara ya pili mfululizo tangu Ligi hiyo ianze kudhaminiwa na Benki ya NBC.

Fiston Mayele na Yanick Bangala wamehitimisha msimu kwa ‘Wananchi’ wakifunga mabao mawili yaliyoipa ushindi timu hiyo dhidi ya Prisons ya Mbeya kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Huu ni mojawapo ya msimu bora kwa timu ya Yanga ikimaliza kwa kushinda mechi nyingi kuliko timu yeyote (25 ) , kutoa sare mitatu, kupoteza miwili na kukusanya alama 78 wakiwazidi watani zao wa jadi Simba kwa alama tano.

Timu hiyo inaelekea mkoani Tanga itakapocheza na timu ya Azam iliyomaliza msimu kwa kuifunga Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro mabao 8-0 kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Juni 12 katika uwanja wa Mkwakwani.

VITA MPYA LIGI KUU NBC

MABAO matano aliyofunga Saido Ntibazonkiza katika ushindi wa mabao 6-1 iliyopata timu ya Simba dhidi ya Polisi Tanzania yameibua ushindani mpya katika kinyang’anyiro cha ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Mabao hayo yamemfanya Saido kufikisha (15) na kumkaribia Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 16.

Saido amefikisha mabao hayo ikiwa ni baada ya kutumikia timu mbili tofauti za Geita Gold katika duru la kwanza na Simba katika duru la pili.

Ushindani huu unaibua shauku kubwa ya kushuhudia michezo ya mwisho kwa vinara hawa ambapo Mayele atacheza dhidi ya Tanzania Prisons huku Saido akicheza na Coastal Union ya Tanga.

SINGIDA BS YAZIDI KUIFUKIA RUVU SHOOTING, AZAM IKITAMBA MKWAKWANI

TIMU ya Singida Big Stars ya Singida imeendelea kuizika timu ya Ruvu Shooting iliyokwisha kushuka daraja baada yankuifunga mabao 2-1.

Ruvu ni timu iliyoshinda michezo michache ya Ligi Kuu ya NBC (Mitano) ikiwa imefunga mabao machache zaidi (19) ikifanikiwa kupata alama 20.

Singida imeendelea kujihakikishia nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao ikikusanya alama 54 katika nafasi ya nne kwenye msimamo.

Matokeo hayo yanaifanya Singida kuwa alama mbili nyuma ya timu ya Azam iliyoshinda mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Mabao yaliyofungwa na Idris Mbombo na Prince Dube yameendela kuiweka Azam nafasi ya tatu huku Coastal ikisalia nafasi ya 10 ikiwa na alama 33.