Category: STORY

PRISONS MAMBO SAFI, MTIBWA IKIILIZA KAGERA

TIMU ya Tanzania Prisons ya Mbeya imejihakikishia nafasi ya kucheza ligi kuu ya NBC msimu ujao baada ya kuifunga KMC ya Dar bao 1-0.

KMC iliyokua na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Singida BS imepoteza kwa bao la mapema kipindi cha kwanza lililofungwa na Edwin Balua.

Prisons imefikisha alama 37 ambazo endapo ikipoteza mchezo wa mwisho haziwezi kufikiwa na timu zilizopo nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.

Mabao ya Vitalis Mayanga, Omary Buzungu na bao la kujifunga la Abdallah Mfuko yameongeza matumaini kwa timu ya Mtibwa kuendelea kusalia Ligi Kuu baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 3-0.

Mtibwa imefikisha alama 32 ikihitaji matokeo ya ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Geita Gold kujihakikishia nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

IHEFU YATAMBA MBARALI, MBEYA CITY NA YANGA HAKUNA MBABE

Timu ya Ihefu imefanikiwa kushinda mchezo katika uwanja wake wa nyumbani wa Highland Estates dhidi ya Geita Gold ikiwa ni baada ya kupita takribani miezi mitatu tangu ilipoifunga Azam bao 1-0.

Geita imepoteza mchezo wa tatu mfululizo na kuruhusu mabao saba katika michezo hiyo huku ikisalia na alama 37 katika nafasi ya sita.

Ukiwa ni ushindi wa tano katika michezo tisa iliyopita kwa Ihefu unaifanya timu hiyo kufikisha alama 36 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Mabao ya Bernard Morison (2) na Salum Abubakar yameifanya timu ya Yanga kutoka nyuma na kuilazimisha sare ya mabao matatu Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mchezo huo ulishuhudia wachezaji Jesus Moloko wa Yanga na Hassan Nassor wa Mbeya City wakishindwa kumaliza mchezo baada ya kuoneshwa kadi nyekundu huku Moloko akitarajiwa kukosa mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho utakaochezwa Tanga Juni 12 kwenye uwanja wa Mkwakwani.

YANGA MGUU MMOJA FAINALI YA SHIRIKISHO

TIMU ya Yanga inayoshika nafasi ya kwanza katika Ligi Kuu ya NBC mpaka mzunguko wa 27 imeendeleza rekodi nzuri ya kushinda mechi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini mabao 2-0.

Mabao yaliyofungwa na mchezaji wa kimataifa wa Burkina Faso Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison wa Ghana yameiweka Yanga nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya fainali katika michuano hiyo.

Yanga imekuwa na rekodi ya kushinda michezo ya Kimataifa kwa asilimia 100 msimu huu ikishinda michezo yote iliyocheza uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hiyo itatupa karata yake ya pili dhidi ya Marumo nchini Afrika Kusini Mei 17 katika uwanja wa Peter Mokaba kwenye Mji wa Polokwane.

Katika mchezo huo wa marudiano Yanga inahitaji ushindi au sare ili kufuzu hatua ya Fainali kwa mara ya kwa katika historia ya timu hiyo kwenye ngazi ya kimataifa.

COSMOPOLITAN MABINGWA FIRST LEAGUE 2022/23

Timu ya Cosmopolitan ya Dar imefanikiwa kutwaa ubingwa wa First League msimu wa 2022/23 baada ya kuifunga Stand United mabao 3-1 kwenye mchezo wa kuhitimisha fainali hizo msimu huu.

Mchezo wa leo ulikua kama kisasi kwa Stand kwani timu hizo zilikutana katika hatua ya makundi kwenye mchezo ambao Stand iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kumaliza kinara katika kundi hilo mbele ya Cosmo.

Cosmo imemaliza mashindano hayo ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi (10) huku ikiwa timu iliyoruhusu mabao mengi pia ya kufungwa (sita).

Cosmo na Stand zimejihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Championship msimu wa 2023/24 baada ya kupanda daraja mbali na Stand kupeteza mchezo wa fainali.

Nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo ya First League hatua ya Nane Bora imeshikwa na Dar City baada ya kuifunga TMA ya Arusha kwa bao 1-0.

Dar City na TMA bado zina nafasi ya kupanda daraja msimu ujao zikilazimika kusubiri ligi ya Championship itakapofika tamati ili kufahamu timu watakazocheza nazo kuwania nafasi ya kushiriki ligi hiyo msimu ujao.

TAKWIMU: FAINALI YA KISASI NANE BORA

FAINALI ya First League hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuchezwa Mei 3, kwenye uwanja wa Azam, Dar es Salaam kati ya Stand United ya Shinyanga na Cosmopolitan ya Dar.

Timu hizi zilikutana hatua ya makundi katika mchezo ambao Stand ilishinda kwa bao moja lililofungwa na Tungu Robert dakika ya 70 kwa mkwaju wa penati.

Timu ya Stand mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote ikiwa imecheza michezo minne katika hatua ya nane bora ikishinda miwili na kutoka sare miwili.

Huku timu ya Cosmopolitan ikicheza michezo minne pia ikishinda miwili, kutoka sare mmoja na kufungwa mchezo mmoja pekee dhidi ya wapinzani wao wa fainali Stand.

Stand imefanikiwa kufunga mabao matano na kuruhusu mabao mawili ya kufungwa huku Cosmo ikifunga mabao saba na kuruhusu mabao matano ya kufungwa.

Fainali hiyo itatanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu saa 9:00 alasiri kati ya Dar City iliyofungwa na Cosmopolitan na TMA FC iliyopoteza mchezo wake wa kwanza wa First League hatua ya nane bora dhidi ya Stand siku ya Mei Mosi.