Category: STORY

NANE BORA FIRST LEAGUE KUTIMUA VUMBI DAR

MICHUANO ya First League hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 24 hadi Mei 3, 2023 michezo yote ikipangwa kuchezwa katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Michuano hiyo inashirikisha timu nne zilizomaliza nafasi za juu katika hatua ya awali kwenye kila kundi ambazo ni African Lyon, Dar City, Cosmopolitan za Dar es Salaam na Lipuli ya Iringa kwa kundi A na Stand United (Shinyanga), TMA FC (Arusha), Rhino Rangers (Tabora) na Alliance FC (Mwanza) kwa upande wa kundi B.

TMA FC ya Arusha haijapoteza mechi yoyote mpaka hatua ya kwanza inakamilika ikishinda mechi saba na kutoka sare saba huku ikiwa ndio timu iliyofunga mabao mengi katika hatua hiyo (29).

Rhino Rangers, Alliance, Lipuli na Dar City zitatafuta nafasi ya kufuzu Ligi ya Championship kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kukosa nafasi hiyo msimu uliopita katika mashindano yaliyochezwa mkoani Mwanza ambapo timu za Mbuni FC (Arusha) na Copco FC (Mwanza) zilipanda daraja.

Mashindano ya mwaka huu yamegawanyika katika makundi mawili yanayoundwa na timu za Stand United, Alliance FC, Cosmopolitan na Lipuli kwa kundi A na African Lyon, Rhino Rangers, TMA, na Dar City kwa kundi B huku timu mbili zitakazomaliza juu kutoka kila kundi zitafuzu nusu fainali na timu mbili zitakazoshinda na kuingia fainali moja kwa moja zitakuwa zimefuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2023/24.

Mashindano hayo yataoneshwa mbashara kupitia Azam TV huku mechi ya ufunguzi ikiwa ni kati ya Stand United na Alliance FC saa 10:00 alasiri ikifuatiwa na mechi kati ya Cosmopolitan na Lipuli saa 1:00 usiku.

DAR ES SALAAM NI NYEKUNDU NA NYEUPE

TIMU ya simba imefanikiwa kushinda mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0 baada ya miaka mitatu tangu wafanye hivyo mwaka 2019.

Simba ikiwa mwenyeji ilifanikiwa kumaliza mchezo kipindi cha kwanza kwa mabao yaliyofungwa na Henock Inonga na Kibu Denis yaliyofanya timu hiyo kufikisha mabao 62 kwa msimu huu.

Mchezo huo ulishuhudia golikipa wa Simba Ally Salum akiibuka shujaa wa mchezo kwa kuokoa nafasi za hatari zilizotengenezwa na Yanga na kumfanya kumaliza mchezo wake wa pili mfululizo bila kuruhusu bao lolote katika Ligi Kuu NBC.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa NBC kwa kufikisha alama 63 na kuisogelea timu ya Yanga yenye alama 68 huku ikisalia michezo minne kabla ya kutamatika kwa Ligi hiyo.

“WANANCHI TUPO TAYARI KUMUUA SIMBA” MUDATHIR YAHYA.

KIUNGO wa timu ya Yanga Mudathir Yahya amejigamba kwa kusema wananchi ni binadamu na kesho wanaenda kupambana na Simba hivyo wapo tayari kuhakikisha wanashinda vita ya kesho ili kuhakikisha wanatwaa ubingwa msimu huu.

“timu ya Simba ina kikosi kizuri ila sisi pia tuna timu nzuri sana ya kupata ushindi kesho, wao wanashambulia vizuri na sisi tunazuia vizuri hivyo mchezo utakua mzuri na tuko tayari kumuua Simba” alisema Mudathir.

Naye kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema kesho ni mechi ya kihistoria ambayo timu nzima imejiandaa kupata matokeo mazuri na wanayo furaha kubwa kuwa na mchezaji kama Fiston Mayele mwenye uwezo wa kubadilisha matokeo muda wowote.

“timu yetu nzima ipo tayari kwa mechi ya kesho kwani ni mechi kubwa na ya kihistoria ambayo ushindi wake utatupa mwanga kuelekea mbio za kutetea kombe letu, mchezaji kama Mayele tunaamini atakua nguzo kubwa kwetu kupata ushindi kwani ameleta tofauti kubwa katika kikosi chetu na kuwa mfano mzuri kwa wachezaji wengine kupambana ili kuinufaisha timu yetu” alisema Kaze.

Yanga inaingia katika mchezo huo siku chache baada ya kushinda mabao 5-0 dhidi ya Kagera Sugar na kuendelea kujiweka kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 68.

“TUNAUTAKA UBINGWA” MOHAMED HUSSEIN.

YAKISALIA masaa machache kabla ya watani wa jadi wa soka la Tanzania timu ya Simba na Yanga kukutana kwenye uwanja wa Mkapa, Dar kesho majira ya saa 11:00 jioni nahodha msaidizi wa Simba Mohammed Hussein amesema wapo tayari kushinda mchezo huo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa Habari kuelekea mchezo huo Mohammed amesema “endapo tukipata alama tatu katika mchezo wa kesho tutakua katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi ili tupambane kwa Pamoja tushinde mchezo huo”

Nahodha huyo amesema pia presha ni kubwa kuelekea mchezo huo kwani hawajafanikiwa kushinda mchezo dhidi ya Yanga kwa kipindi kirefu hivyo wapo tayari kupambania nembo ya timu yao kuhakikisha wanarudisha heshima dhidi ya watani zao wa jadi.

“Unaposhindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya mpinzani wako mkuu inaibua mijadala mingi sana na hiyo ni mojawapo ya sababu kuu inayotupelekea kesho tupambane kushinda mechi hiyo” alisema Mohammed.

DABI YA DAR ES SALAAM.

IMESALIA Siku moja pekee kwa miamba ya soka nchini Tanzania Simba na Yanga kukutana katika mchezo wa duru la pili katika Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa majira ya 11:00 jioni kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam jumapili Aprili 16 .

Fiston Mayele wa Yanga ndiye kinara wa kufunga mabao katika michezo ya Ligi Kuu akifunga 16 huku akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.

Said Ntibazonkiza ndiye mchezaji aliehusika katika mabao mengi kwenye Ligi Kuu ya NBC (19) akifunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao tisa huku akifuatiwa na Fiston Mayele wa Yanga aliehusika katika mabao 18 akifunga 16 na kutoa pasi mbili za mabao.

Timu hizo zinakutana Simba ikiwa kinara wa kufunga mabao katika Ligi Kuu NBC ikifunga mabao 60 huku Yanga ikishika nafasi ya pili na mabao 50.