Category: STORY

RHINO YAANZA KIBABE, TMA IKIENDELEZA REKODI

TIMU ya Rhino Rangers ya Tabora imeanza kibabe mashindano ya First League hatua ya Nane Bora kwa kutoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya African Lyon ya Dar kwenye mchezo wa kundi B uliopigwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Azam.

Pamoja na African Lyon kutangulia kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Agiri Ngoda walishindwa kuhimili mashambulizi ya Rhino waliosawazisha kupitia kwa Ramadhan Abdallah na kupata bao la ushindi dakika ya mwisho lililofungwa na Masawe Masawe.

TMA Stars ya Arusha ilicheza na Dar City ya Dar es Salaam saa 1:00 usiku ikiwa ni mchezo wa pili wa kundi B uliomalizika kwa suluhu.

TMA imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa First League msimu huu mpaka kufikia hatua ya Nane Bora huku ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache (9).

Rhino Rangers baada ya ushindi wa leo wanashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi B wakifuatiwa na Dar City na TMA wenye alama moja kila timu baada ya sare ya leo huku nafasi ya mwisho ikishikwa na African Lyon.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 26 kwa michezo miwili ya kundi A itakayokutanisha timu za Lipuli dhidi ya Alliance mchezo wa saa 10:00 alasiri na Cosmopolitan itakua mwenyeji wa Stand United saa 1:00 usiku.

PRISONS YAMALIZA UBABE WA GEITA NYANKUMBU

TIMU ya Prisons ya Mbeya imemaliza ubabe wa Geita Gold ikicheza katika uwanja wake wa Nyankumbu kwa kuifunga Mabao 3-1.

Mchezo wa mwisho kwa Geita kufungwa uwanja wa Nyankumbu kabla ya kipigo cha leo ilikua dhidi ya timu ya Pamba kutoka Mwanza katika mchezo wa Ligi ya Championship msimu wa 2020/21.

Mabao ya Jeremiah Juma, Samson Mbangula na Edwin Balua yameifanya Prisons kuwa timu ya kwanza kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Geita Gold kwenye uwanja wa Nyankumbu tangu timu hiyo ipande daraja.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa timu ya Prisons ikipanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 31.

ALLIANCE, LIPULI ‘MWANZO MGUMU’ NANE BORA

TIMU za Alliance Fc ya Mwanza na Lipuli ya Iringa zimeanza mashindano ya First League hatua ya Nane Bora vibaya baada ya kupoteza michezo yao ya ufunguzi.

Alliance ilipoteza dhidi ya Stand United ya Shinyanga kwa mabao 2-0 huku Lipuli ikifungwa na Cosmopolitan ya Dar es Salaam kwa mabao 3-1.

Timu za Alliance na Lipuli zilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki hatua ya nane bora msimu uliopita Mkoani Mwanza huku zikifungwa na timu ngeni katika hatua hiyo msimu huu.

Cosmopolitan wanakwea nafasi ya kwanza kwenye kundi A wakiwa na Idadi kubwa ya mabao ya kufunga (3) dhidi ya Stand yenye mabao (2).

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 25 kwa michezo miwili ya Kundi B timu ya African Lyon ya Dar ikiikaribisha Rhino Rangers saa 10:00 alasiri na TMA ya Arusha ikiwa mwenyeji wa Dar City ya Dar saa 1:00 usiku huku michezo yote ikipigwa uwanja wa Azam Dar na kuonyeshwa Mbashara kupitia kituo cha televisheni cha Azam.

KMC, RUVU SHOOTING, HALI NI TETE

MCHEZO wa Ligi Kuu NBC kati ya Dodoma Jiji dhidi ya KMC umemalizika kwa kushuhudia kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akianza mchezo wake wa kwanza kama kocha mkuu wa KMC kwa kufungwa bao 1.

Bao la Dodoma Jiji limefungwa dakika ya 19 na mshambuliaji Collins Opare aliefikisha mabao saba na kuendelea kuididimiza KMC nafasi ya 14 ikisalia na alama 26.

Katika mechi 2 za msimu huu walizokutana zote Dodoma Jiji imepata ushindi, mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Uhuru, Dar es salaam, Dodoma Jiji waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Azam FC baada ya kuifunga Mtibwa Sugar 2-1 nyumbani imefanikiwa kushinda mechi ya pili mfululizo katika Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 ugenini.

Ruvu Shooting Imeendelea kupoteza matumaini ya kusalia Ligi Kuu msimu ujao baada ya kushinda mechi mbili pekee kati ya 10 mfululizo zilizopita ikikusanya alama 20 katika nafasi ya mwisho kwenye msimamo.

JKT TANZANIA YATINGA LIGI KUU YA NBC

SARE ya bao moja iliyopata timu ya Pamba kutoka mkoa wa Mwanza dhidi ya Mbuni ya Arusha leo imeihakikishia JKT Tanzania kupanda Ligi Kuu licha ya kupoteza mchezo wake ugenini mbele ya Kitayosce ya Tabora kwa mabao 3-2.

JKT inarudi Ligi Kuu ya NBC ikiwa na michezo mitatu mkononi huku vita ikibaki kwa Kitayosce na Pamba kusaka mmoja wa kuungana na Maafande hao kupanda moja kwa moja bila kucheza hatua ya mtoano.

Iwapo Pamba itashinda mechi zote zilizobaki itafikisha pointi 61 huku Kitayosce nayo ikishinda zote itafikisha alama 62.

Ushindi wa Kitayosce umeiweka nafasi ya pili kwa alama 53, huku Pamba wakishuka Hadi nafasi ya tatu kwa pointi 52 na timu zote zimebakiza mechi tatu kuamua hatma yao.