MICHUANO ya First League hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 24 hadi Mei 3, 2023 michezo yote ikipangwa kuchezwa katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Michuano hiyo inashirikisha timu nne zilizomaliza nafasi za juu katika hatua ya awali kwenye kila kundi ambazo ni African Lyon, Dar City, Cosmopolitan za Dar es Salaam na Lipuli ya Iringa kwa kundi A na Stand United (Shinyanga), TMA FC (Arusha), Rhino Rangers (Tabora) na Alliance FC (Mwanza) kwa upande wa kundi B.
TMA FC ya Arusha haijapoteza mechi yoyote mpaka hatua ya kwanza inakamilika ikishinda mechi saba na kutoka sare saba huku ikiwa ndio timu iliyofunga mabao mengi katika hatua hiyo (29).
Rhino Rangers, Alliance, Lipuli na Dar City zitatafuta nafasi ya kufuzu Ligi ya Championship kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kukosa nafasi hiyo msimu uliopita katika mashindano yaliyochezwa mkoani Mwanza ambapo timu za Mbuni FC (Arusha) na Copco FC (Mwanza) zilipanda daraja.
Mashindano ya mwaka huu yamegawanyika katika makundi mawili yanayoundwa na timu za Stand United, Alliance FC, Cosmopolitan na Lipuli kwa kundi A na African Lyon, Rhino Rangers, TMA, na Dar City kwa kundi B huku timu mbili zitakazomaliza juu kutoka kila kundi zitafuzu nusu fainali na timu mbili zitakazoshinda na kuingia fainali moja kwa moja zitakuwa zimefuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2023/24.
Mashindano hayo yataoneshwa mbashara kupitia Azam TV huku mechi ya ufunguzi ikiwa ni kati ya Stand United na Alliance FC saa 10:00 alasiri ikifuatiwa na mechi kati ya Cosmopolitan na Lipuli saa 1:00 usiku.