Category: STORY

SIMBA ‘YAIBAMIZA’ KENGOLD LIGI KUU YA NBC

TIMU ya KenGold imeshindwa kutamba nyumbani kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora baada ya kufungwa na timu ya Simba mabao 0-5 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ilimchukua dakika 20 mchezaji wa Simba Kibu Denis kufungua ukurasa wa mabao huku Ellie Mpanzu akiongeza bao la pili dakika ya 22 ya mchezo huo na dakika ya 25 Kibu Denis alirejea tena nyavuni kuongeza bao la tatu kwa timu yake na kuifanya kuwa mbele kwa mabao matatu.

Dakika ya 36 ya mshambuliaji wa Simba Leonel Ateba aliiongezea timu yake bao la nne na kufanya mchezo huo Kwenda mapumziko ubao ukisomeka 0-4.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya KenGold kujaribu kusaka mabao ili kuweka mzani sawa lakini dakika ya 75 mchezaji wa Simba Jean Ahoua aliongeza bao kwa timu yake hivyo mchezo kutamatika kwa ubao kusomeka 0-5.

Kibu Dennis aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo huku Jean Ahoua akiongeza wigo wa mabao akifikisha bao la 16 msimu huu na kuendelea kushikilia usukani wa vinara mabao.

LIGI KUU NBC KUREJEA JUNI 18.

LIGI Kuu ya NBC inarejea juni 18 ikiwa ni mzunguko wa 29 huku michezo yote hiyo itakayochezwa viwanja mbali mbali ikitarajiwa kuanza saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa kwanza utachezwa uwanja wa CCM kirumba Pamba Jiji inayotafuta uhakika wa kusalia Ligi Kuu ya NBC itaikaribisha timu ya JKT Tanzania, huku Namungo ikiikaribisha Kagera Sugar iliyoshuka daraja katika uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Timu ya Dodoma Jiji itakuwa mwenyeji wa timu ya Singida Black Stars katika uwanja wa Jamhuri Dodoma na Mashujaa itaialika KMC katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Kwa upande wa KenGold iliyoshuka daraja itakuwa mwenyeji wa timu ya Simba inayowania ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora huku Tanzania Prisons ikiialika timu ya Young Africans katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Azam itakuwa mwenyeji wa Tabora United katika uwanja wa Azam Complex uliopo jijini Dar es Salaam na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Coastal Union na Fountain Gate katika uwanja wa Mkwakwani uliopo mkoani Tanga.

KARIAKOO DERBY

KARIAKOO ‘DERBY’ KUPIGWA JUNI 25.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeusogeza mbele mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya klabu ya Yanga na klabu ya Simba ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 15, 2025 kuanzia saa 11:00 jioni.

Mchezo huo sasa utafanyika Juni 25, 2025 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Bodi inazitakia maandalizi mema klabu za Yanga na Simba kuelekea mchezo huo.

YOUNG AFRICANS, SIMBA ‘HAWAFUNGIKI’ UGENINI LIGI KUU YA NBC.

KLABU za Simba na Young africans ni timu pekee za Ligi Kuu ya NBC ambazo hazijafungwa kwenye mchezo wowote wa ugenini msimu huu zikicheza michezo 27 kila moja.

Young Africans katika msimu huu wa Ligi Kuu imefanikiwa kucheza michezo 14 viwanja vya ugenini na kufanikiwa kushinda michezo 13 huku ikipata sare moja na ikivuna alama 40 ikiweka ‘kimiani’ mabao 35 na kuruhusu mabao mawili pekee.

Kwa upande wa timu ya Simba imefanikiwa kucheza michezo 13 ugenini ikishinda michezo 12, sare moja na kuvuna alama 37 baada ya kufunga mabao 25 na kuruhusu mabao manne pekee.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea juni 15 kwa mchezo wa dabi ya Kariakoo ambapo timu ya Young Africans itakuwa mwenyeji wa timu ya Simba katika uwanja wa Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam saa 11:00 jioni.

HAWA HAPA WAKALI WA KUPIKA MABAO LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa Simba Jean Ahoua ameendeleza ubabe akihusika katika mabao mengi zaidi kuliko wachezaji wengine wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 hadi sasa.

Ahoua ambaye amejiunga na Simba mwanzoni mwa msimu amefanikiwa kufunga mabao 15 na kutoa pasi za mabao nane hivyo kuhusika katika mabao 23.

Prince Dube wa Young Africans anashika nafasi ya pili baada ya kuhusika katika mabao 21 akifanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani mara 13 na kutoa pasi za mabao nane ikiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya timu hiyo akitokea Azam FC.

Pacome Zouzoua wa Young Africans nae hajabaki nyuma akiwa amefanikiwa kuhusika katika mabao 18 baada ya kufunga mabao 9 na kutoa pasi za mabao 9.

Kwa upande wake Feisal Salum wa timu ya Azam amehusika katika mabao 17 akiwa ametoa pasi za mabao 13 na kufunga mabao 6 huku akiwa kinara wa kutoa pasi za mabao.