Category: STORY

AZAM YALIPA KISASI KWA TABORA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Azam imeshusha kipigo kizito cha mabao 5-0 kwa timu ya Tabora United na kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 na timu hiyo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Dakika 11 zilimtosha Abdul Suleiman ‘Sopu’ kufungua ukurasa wa mabao kwa timu yake huku winga wa timu hiyo Gibril Sillah akiiongezea timu yake mabao mawili dakika ya 16 na 29 na dakika ya mwisho ya kipindi cha kwa Iddy Nado aliongeza jingine hivyo Azam Kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.

Kipindi cha pili Tabora walionyesha nia ya kutafuta bao kwa mashambulizi kadhaa kabla ya ndoto yao ‘kudidimizwa’ dakika ya 89 na mshambuliaji wa Azam Nassor Saadun ambaye aliongeza bao kwa timu yake na kufanya mchezo huo kutamatika kwa mabao 5-0.

Mabao mawili ya Gibril Sillah aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo yanamfanya kufikisha jumla ya mabao 11 sawa na Pacome Zouzoua wa Young Africans kwenye msimamo wa vinara wa mabao.

COASTAL UNION YAGEUZA MKWAKWANI ‘MACHINJIONI’ LIGI KUU YA NBC.

‘WAGOSI wa kaya’ timu ya Coastal Union imefanikiwa kupanda ushindi wa tatu mfululizo kwenye uwanja wake wa Mkwakwani tangu kukamilika marekebisho yake baada ya kuifunga timu ya Fountain Gate 1-0.

Lucas Kikoti ndiye aliyepeleka furaha kwa wakazi wa mkoa wa Tanga akifunga kwa mkwaju wa penati uliopatikana kipindi cha pili.

Tangu uwanja huo urejeshwe kwenye matumizi Coastal imezifunga timu za Singida Black Stars kwa mabao 2-1, Ken Gold 2-1 na ushindi wa jana unakamilisha mchezo wa tatu mfululizo wakitumia uwanja huo wakiwa hawajapoteza wala kutoa sare.

Coastal imefikisha alama 34 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 huku ikisalia na mchezo mmoja kukamilisha msimu.

Bakari Msimu wa Coastal Union aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango bora zaidi ya wachezaji wenzake.

‘MAAFANDE’ WASHINDWA KUTAMBA KWA ‘WANANCHI’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tanzania Prisons imeshindwa kuonyesha ubabe ikicheza uwanja wa nyumbani wa Sokoine, Mbeya baada ya kukubali kipigo cha mabao 0-5 kutoka kwa Young Africans.

Ilimchukua dakika 31 Mudathir Yahya kuiandikia Young Africans bao la kuongoza kabla ya dakika tatu baadae Clatous Chama kuongeza msumari wa pili na kuwafanya ‘Wananchi’ kwenda mapumziko wakiongoza mabao 0-2.

Dakika 11 baada ya kipindi cha pili kuanza Pacome Zouzoua aliongeza ‘chuma’ cha tatu huku dakika nne baadae Israel Mwenda akaongeza la nne kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya Chadrack Boka na dakika ya 75 Pacome aliingia kambani tena na kukamilisha karamu ya mabao kwa Young Africans.

‘Wananchi’ wameendelea kujikita kileleni baada ya ushindi huo wakifikisha alama 76 huku wakiwa wamefunga mabao 76 wakifuatiwa na timu ya Simba yenye alama 75 wakifunga mabao 68 huku timu hizo zikisalia na michezo miwili kutamatisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC.

Pacome Zouzoua aliibuka nyota wa mchezo na kukabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi akifunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kupata alama tatu.

MASHUJAA,KMC HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mashujaa imeshindwa kubaki na alama zote tatu nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na timu ya KMC kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma.

Mchezo ulianza kwa kila timu kupambania timu yake na dakika ya 11 Mundhur Vuai wa Mashujaa aliifungia timu yake bao la kuongoza na kuwanyanyua mashabiki wa Mashujaa waliojitokeza uwanjani.

Ikisalia dakika moja mchezo kumalizika huku Mashujaa ikiamini imeshakusanya alama zote tatu mchezaji Akramu Muhina aliisawazishia KMC na kufanya timu hizo kugawana alama.

Mashujaa imesalia nafasi ya 7 na alama 34 huku KMC ikiwa na alama 34 kwenye nafasi ya 10 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.Akram Muhina wa KMC ndiye aliibuka mchezaji bora wa mchezo baada ya kuiokoa timu yake kwa bao la ugenini na kuipa tiketi ya Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

JKT YASHINDWA KUFURUKUTA UGENINI LIGI KUU YA NBC

MZUNGUKO wa 29 ulibaki na kicheko kwa timu ya Pamba jiji ilipokuwa mwenyeji wa JKT Tanzania mkoani Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuchomoza na ushindi ‘finyu’ wa bao 1-0 nyumbani.

Dakika ya 40 zilitosha kwa timu ya Pamba jiji kupata uongozi kwa bao lililofungwa na Zabona Mayombya.

Pamba jiji imejiweka nafasi ya 11 ikiwa na alama 33 huku JKT Tanzania ikisalia nafasi ya 6 na alama zake 35.

Katika mchezo huo mchezaji wa Pamba jiji Zabona Mayombya aliyefunga bao pekee alichaguliwa kuwa mchezaji bora na nyota wa mchezo huo.