Category: STORY

TMA YAJIPATA KWA GEITA GOLD NBC CHAMPIONSHIP

LIGI ya NBC Championship Mzunguko wa 16 ulianza jana januari 24 kwa michezo ilicho  na leo imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa mkoani Arusha Katika Uwanja wa Sheikh Amri  Abeid majira ya  saa kumi jioni.

Katika mchezo huo timu ya TMA waliwakaribisha Geita Gold ambapo mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa kasi  kubwa ambapo mpaka mapumziko hakuna aliyeweza kutikisa nyavu za mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa ambapo TMA walifanikiwa kupata bao la kwanza ikiwa ni dakika ya 50 ya mchezo huo  kupitia mchezaji wao Abdul Shahame kabla ya Kasimu Shaibu kuongeza bao  la pili dakika ya 61 ya mchezo huo .

Dakika ya 72 ya mchezo huo Geita Gold walifanikiwa kupata goli lao la kwanza kupitia mchezaji wao Masanja Jesto  hivyo matokeo kuwa 2-1 ambayo yalisalia mpaka mwisho wa mchezo huo.

Baada ya mchezo huo kutamatika TMA alifanikiwa kufikisha pointi 30 hivyo kupanda hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi hiyo kutoka nafasi ya sita alipokuwa awali.

Ligi ya NBC Championship itaendelea kesho kwa michezo minne Bigman dhidi ya Mbeya City ulioahirishwa kuchezwa leo kutokana na mvua kubwa kunyesha katika uwanja wa Ilulu Lindi,Stand United dhidi ya Kiluvya,Transit Camp dhidi ya Biashara United na Mbuni dhidi ya Polisi Tanzania.

MTIBWA HASHIKIKI NBC CHAMPIONSHIP.

 

LIGI ya NBC Championship Mzunguko wa 16 ulianza jana Januari 24 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mkoani Mtwara, Mbeya kwanza iliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Songea United, ushindi ulioipandisha Mbeya kwanza hadi nafasi ya nne kwenye msimamo ikifikisha alama 30.

African Sports ya Tanga iliifunga Cosmopolitan ya Dar es salaam kwa mabao 2-1 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa TFF Center mkoani Tanga.

Mtibwa Sugar ikiwa ugenini Mkoani Pwani ikaifunga Green Warriors kwa mabao mawili kwa moja mchezo ambao ulichezwa katika uwanja wa Mabatini.

Ushindi huo wa Mtibwa unaifanya kufikisha alama 41 na kuendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Champiomship ya NBC kwa tofauti ya alama saba na timu inayomfuatia Mbeya City.

NBC CHAMPIONSHIP MZUNGUKO WA 16 KUPIGWA MIKOA MITATU LEO.

MZUNGUKO wa 16 wa Ligi ya Championship ya NBC unaanza kuchezwa leo Januari 24 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha Mbeya Kwanza dhidi ya Songea United kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa pili utazikutanisha African Sports dhidi ya Cosmopolitan kwenye uwanja wa TFF Center, Mnyanjani – Tanga kuanzia saa 10 alasiri.

Mkoani Pwani Green Warriors itaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Mabatini mchezo ambao utachezwa kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mtibwa Sugar ndio kinara wa Ligi ya Championship ya NBC mpaka sasa ikiwa na alama 38 kwenye michezo 15 ya kwanza huku Biashara United ikiburuza mkia ikiwa na alama moja baada ya michezo 15.

LIGI KUU NBC YA NNE KWA UBORA AFRIKA

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.

Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 hadi nafasi ya nne ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.

Kwa mujibu wa taarifa ya IFFHS kwa upande wa Afrika nchi zilizoko chini ya Shirikisho la Soka (CAF) Ligi Kuu ya Misri inayofahamika kama Nile Premier League ndio kinara kwa ubora Afrika.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Botola Pro ambayo ni Ligi Kuu ya Morocco huku League 1 ya Algeria ikishika nafasi ya tatu kwa ubora mwaka 2024.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania imekwea hadi nafasi ya nne barani Afrika kutokana na ligi hiyo kuwa na usimamizi bora kuanzia Serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Klabu zinazoshiriki ligi hiyo, wadhamini mbalimbali wanavyounga mkono pamoja na mashabiki.

HAWA HAPA WASHINDI WA TUZO ZA NBC DESEMBA.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Yanga Sead Ramovic akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Mzize amewashinda Prince Dube wa Yanga na Feisal Salum wa Azam alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 4 na kutoa pasi za mwisho 3 katika dakika 288 alizocheza ndani ya mwezi huo.

Yanga ilizifunga Tanzania Prisons mabao 4-0, Dodoma Jiji 0-4 Mashujaa 3-2, na Fountain Gate mabao 5-0 hivyo kukusanya alama 12.

Aidha Kocha wa Yanga Sead Ramovic amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Davis Fadlu wa Simba na Rachid Taoussi wa Azam baada ya kuiongoza Yanga kushinda michezo minne ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar es Salaam, Ashraf Omar kuwa Meneja bora wa uwanja mwezi desemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.

Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC kamati imemchagua mchezaji wa Mbeya City, Kilaza Mazoea kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo kwa mwezi desemba baada ya kufunga mabao manne katika dakika 234 alizocheza akiwashinda Elias Maguri wa Geita Gold/Biashara na Emmanuel Maziku wa Stand United.

Kocha wa Mbeya City Salum Mayanga, amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi desemba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo 3 na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo akiwashinda Awadh Juma wa Mtibwa na Maka Mwalwisi wa TMA alioingia nao fainali.

Mbeya City walizifunga timu za Polisi Tanzania 4-0,Geita Gold 1-0 na Cosmopolitan 1-0.