Category: STORY

MZIZIMA DERBY HAKUNA MBABE.

 

MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC Simba dhidi ya Azam umemalizika kwenye uwanja wa CCM KIRUMBA mkoani Mwanza kwa sare ya Bao 1.

Prince Dube anaendelea kuwa mwiba mkali kwa Simba kwenye michezo ya hivi karibuni kutokana na kufunga kwenye michezo mfululizo wanapokutana na Simba hii ni baada ya kufunga goli la uongozi kwa Azam Dakika ya 14 ya mchezo.

Chama anaendelea kuwa msaada mkubwa kwa Simba baada ya kufunga bao lililoipatia Simba alama moja Dakika 90+1 ya mchezo na kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1.

Azam inaendelea kusalia nafasi ya pili na alama 32 kwenye michezo 14 huku simba ikisalia nafasi ya 3 na alama 30 kwenye michezo 13 ikibakiwa na mchezo wa ‘kiporo’ dhidi ya Geita Gold utakaopigwa Februari 12.

MZIZIMA DERBY KUPIGWA LEO CCM KIRUMBA.

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea Leo kwa mchezo mmoja kuchezwa kati ya Simba na Azam “Mzizima Derby” kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza saa 10:00 alasiri.

Simba inaingia kwenye mchezo Huu ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo na alama 29 kwenye michezo 12 huku Azam ikiwa nafasi ya pili ikiwa na alama 31 kwenye michezo 13.

Ni kwa mara ya kwanza mchezo Huu wa Derby ndani ya Ligi Kuu ya NBC kupigwa katika mkoa wa Mwanza na fursa kwa wana Mwanza kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ndani ya ardhi yao kwani hakuna timu yoyote kutoka mwanza inayoshiriki ligi hiyo.

KENGOLD KUENDELEA KUJICHIMBIA KILELENI NBC CHAMPIONSHIP LEO ?

 

NBC Championship mzunguko wa 21 unaanza Leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye kwenye mikoa miwili ya Pwani na Morogoro.

Mkoani Pwani Pan African itaikabili KenGold saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Mabatini, KenGold inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na alama 44 kwenye michezo 20 iliyocheza mzunguko huu unaweza kuamua ni nani atakayeongoza usukani wa msimamo wa NBC championship kutokana na alama za timu zinazofuatia, Hivyo ushindi kwenye mchezo huu utamhakikishia kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo.

Mchezo mwengine mkoani Morogoro Transit Camp itaialika Copco kwenye uwanja wa Jamhuri saa 10:00 alasiri, Transit Camp ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na alama 19 huku Copco ikiwa nafasi ya 15 ikiwa na alama 13 hivyo kila timu ikiwa na uhitaji wa alama kujinasua kwenye nafasi iliyopo.

YANGA KUIVAA MASHUJAA LIGI KUU YA NBC LEO.

 

LIGI Kuu ya NBC inaendelea Leo Februari 8 kwa mchezo mmoja Kati ya Yanga dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Dodoma Jiji huku Mashujaa ikipoteza kwenye mchezo wao dhidi ya Simba.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 34 kwenye michezo 13 huku Mashujaa ikiwa nafasi ya 15 kwenye mstari wa kushuka daraja na alama zake tisa kwenye michezo 13.

NBC CHAMPIONSHIP YAPAMBA MOTO.

 

MZUNGUKO wa 20 ligi ya NBC Championship umemalizika na kushuhudia jumla ya michezo nane ikichezwa huku mabao 22 yakifungwa.

KenGold inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 43 kwenye michezo 20 huku Pamba na Biashara United zikifuatia zikiwa na alama 43 kila moja zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Ruvu Shooting yenye maskani yake mkoani Dodoma kwasasa inaendelea kuburuza mkia kwenye msimamo ikiwa na alama nne pekee kwenye michezo 20 iliyocheza ikifunga mabao nane na kufungwa 41.