Category: STORY

KENGOLD HASHIKIKI NBC CHAMPIONSHIP.

 

MZUNGUKO wa 23 wa Ligi ya NBC Championship umemalizika na kushuhudiwa jumla ya mabao 15 yakifungwa kwenye michezo 8.

kenGold inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo ikıwa na alama 53 tofauti ya alama nne na timu ya Biashara United huku kila timu ikisalia na michezo saba.

Biashara United inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 49 ikifuatiwa na Pamba yenye alama 48 huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Mbeya Kwanza yenye alama 46.

Ruvu Shooting inaendelea kusota nafasi ya mwisho kwenye msimamo licha ya ushindi wake iliyoupata dhidi ya Copco ikiwa na alama 11 kwenye michezo 23.

TANZANIA KINARA IDADI YA TIMU ZILIZOTINGA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA.

 

WAWAKILISHI wawili wa Ligi Kuu ya NBC Simba na Yanga wameipaisha Tanzania katika historia ya kuwa nchi pekee Afrika iliyoingiza timu mbili hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/2024.

Yanga imeingia hatua ya robo fainali baada ya kujikusanyia alama nane kwenye michezo sita ikishinda michezo miwili ikipata sare kwenye michezo miwili na kufungwa michezo miwili huku Simba ikiingia hatua hii na alama tisa kwenye michezo sita ikishinda miwili ikipata sare michezo mitatu na kufungwa mchezo mmoja pekee.

Yanga inatarajiwa kukutana na Mamelodi Sundowns, Petro de Luanda au Asec Mimosas huku Simba ikitarajiwa kukutana na Al Ahly, Petro de Luanda au Mamelodi Sundowns.

Hatua ya robo fainali itachezwa Kati ya Machi 29-31 kwa timu zote mbili kuanzia kwenye uwanja wa Nyumbani Benjamin Mkapa.

KENGOLD, BIASHARA VINARA WA USHINDI NBC CHAMPIONSHIP.

 

TAYARI mizunguko 22 ya Ligi ya NBC Championship sawa na michezo 176 imeshachezwa na Kushuhudiwa jumla ya mabao 401 yakifungwa.

KenGold na Biashara United ndiyo timu zinazoongoza kwa kushinda michezo mingi kwenye Ligi ya NBC Championship zikifanya hivyo mara 15 kila mmoja huku KenGold ikifunga mabao 37 na kuruhusu mabao 12 na kufikisha alama 50 kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo wakati Biashara ikifunga mabao 38 na kufungwa mabao 14 ikiwa na alama 49 katika nafasi ya pili kwenye msimamo.

Pamba na Mbeya Kwanza zinafuatia zikishinda michezo 14 kila mmojahuku Pamba ikishika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na alama 47 ikifunga mabao 35 na kuruhusu 12 wakati Mbeya Kwanza ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 45 ikifunga mabao 35 na kuruhusu mabao 22.

Ruvu Shooting imeshinda mchezo mmoja pekee kwenye michezo 22 waliyocheza hadi hivi sasa wakifunga mabao 11 na kuruhusu 43 ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo.

RUVU YAONJA RADHA YA USHINDI NBC CHAMPIONSHIP, PAMBA YABANWA MABATINI.

 

MICHEZO mitatu ya Ligi ya NBC Championship mzunguko wa 21 imechezwa kwenye mikoa mitatu tofauti.

Ruvu Shooting kwa mara ya kwanza ndani ya NBC Championship inaondoka na alama tatu baada ya kuifunga Mbuni mabao 2-1 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma mchezo uliopigwa saa 8:00 mchana, Ruvu Shooting imewachukua michezo 21 kusubiri alama tatu za kwanza ndani ya Ligi ya NBC Championship.

Mkoani Pwani kwenye uwanja wa Mabatini saa 10:00 alasiri Green Warriors ikaialika Pamba na mchezo huo kumalizika kwa suluhu.

Mchezo wa mwisho kwa leo ukazikutanisha Stand United dhidi ya Polisi Tanzania kwenye uwanja wa Mwadui Complex na kumalizika kwa Polisi Tanzania kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

DODOMA, PWANI, SHINYANGA NBC CHAMPIONSHIP INAPIGWA LEO.

 

NBC Championship mzunguko wa 21 inaendelea leo kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye MIKOA ya Dodoma, Pwani na Shinyanga.

Mkoani Dodoma Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Mbuni saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Jamhuri.

Ruvu Shooting ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo na alama nne huku Mbuni ikiwa nafasi ya sita na alama 37.

Mkoani Pwani Green warriors itaialika Pamba kwenye uwanja wa mabatini saa 10:00 alasiri, Green warriors inashika nafasi ya 11 na alama 20 huku Pamba ikiwa nafasi ya pili na alama 43.

Mchezo wa mwisho kwa leo utazikutanisha Stand United dhidi ya Polisi Tanzania saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.