Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Juni 2, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Ligi Kuu ya NBC
Mechi Namba 190: Simba SC 2-1 Mashujaa FC
Mchezaji wa klabu ya Mashujaa, Seif Abdallah amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kurusha chupa za maji kuelekea kwa mashabiki huku pia akionekana mara kadhaa akiingia kiwanjani kumlalamikia mwamuzi wa mchezo akitokea katika benchi la timu hiyo kwenye uwanja wa KMC Complex Mei 2, 2025.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mtunza vifaa wa klabu ya Mashujaa, Juma Nyenje amefungiwa miezi sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kurusha chupa za maji kuelekea kwa mashabiki kwenye uwanja wa KMC Complex Mei 2, 2025 wakati mchezo tajwa hapo juu ukiendelea.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:3 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.
Mechi Namba 218: JKT Tanzania 3-1 Fountain Gate
Klabu ya Fountain Gate imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia badala yake walitumia eneo la nje ya chumba kwa shughuli hiyo kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 220: Simba SC 1-0 Singida Black Stars
Kocha wa viungo wa Klabu ya Simba, Riedoh Berdien ameadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuanzisha vurugu kwa kurusha koni kwenye benchi la ufundi la Singida Black Stars walipokuwa wameketi maofisa wa ufundi na wachezaji wa akiba wa klabu hiyo.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Klabu ya Simba imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa za maji kiwanjani wakati wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa KMC Complex Mei 28, 2025.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mchezaji wa klabu ya Singida Black Stars, Jonathan Sowah ameadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuwaonesha ishara ya matusi mashabiki wa klabu ya Simba waliokuwa jukwaani, pamoja kitendo chake cha kung’oa kibendera cha kona.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Hery Sasii amefungiwa miezi sita (6) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo huo baada ya kufanya maamuzi mengi yaliyoashiria kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za mpira wa miguu.Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Kocha wa klabu ya Simba, Fadlu Davis ametozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kuishutumu Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuwa ina ajenda tofauti kuhusiana na ratiba ya michezo ya klabu hiyo kwenye Ligi Kuu ya NBC. Fadlu alizungumza hayo alipokuwa anafanya mahojiano na Azam TV baada ya kumalizika kwa mchezo tajwa hapo juu, akionesha kutoridhishwa na ratiba ya michezo ya Ligi ya klabu yake.Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Mechi Namba 222: Tanzania Prisons 2-1 Coastal Union
Klabu ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la watoto waokota mipira (Ball Kids) kuficha na kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani.
Kuanzia dakika ya 74 ya mchezo baada ya Tanzania Prisons kufunga bao la pili, watoto hao walikuwa wakificha mipira inayotoka hali iliyosababisha kuwa na upungufu mkubwa wa mipira licha ya jitihada kubwa za kuwaonya watoto hao.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Ligi ya Championship ya NBC
Mechi Namba 223: Geita Gold 2-3 Mbeya City
Klabu ya Mbeya City imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.Hii ni mara ya nne kwa klabu ya Mbeya City kutenda kosa hili katika msimu wa 2024/2025. Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba PO1: Transit Camp 3-2 Kiluvya FC
Klabu ya Kiluvya imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa TFF Center, Kigamboni Mei 15, 2025.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba PO5: Geita Gold 2-2 Stand United
Klabu ya Geita Gold imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la mashabiki wake kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita Mei 24, 2025.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewaondoa kwenye ratiba ya michezo ya Ligi na kupeleka shauri lao Kamati ya Maadili ya TFF, waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu ambao ni mwamuzi wa kati Japhet Smart (Katavi), mwamuzi msaidizi namba moja, Abdallah Malimba (Dar es Salaam), mwamuzi msaidizi namba mbili, Ramadhani Kiloko (Tanga) na mwamuzi wa akiba, Mangile Hobu (Geita).
Licha ya kufanya maamuzi kadhaa ya utata yaliyoonesha wazi kushindwa kwao kutafsiri sheria 17 za mpira wa miguu katika mchezo huo, waamuzi hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo, jambo ambalo likithibitika watachukuliwa hatua zaidi za kikanuni pamoja na watu wengine wote waliohusika.Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.1) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mechi Namba PO6: Stand United 2-0 Geita Gold
Klabu ya Stand United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la walinzi wake wa uwanjani (stewards) na baadhi ya mashabiki wao kuwafanyia vurugu viongozi wa klabu ya Geita Gold na kuwazuia kuingia uwanjani kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga Mei 29, 2025.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Stand United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kushindwa kuandaa uwanja kikamilifu kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga Mei 29, 2025 kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:48 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Stand United walifunga madirisha ya vyumba vya kuvalia kwa kutumia misumari maalum iliyowekwa kwa kutumia mashine, jambo ambalo lilisababisha madirisha hayo kushindwa kufunguka na kufanya vyumba hivyo kukosa hewa na mwanga wa kutosha.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu ya Stand United imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la watoto waokota mipira (Ball Kids) kuficha na kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani wakati mchezo tajwa hapo juu ukiendelea kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, jambo lililotafsiriwa kama hila ya kupoteza muda.Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
First League
Mechi Namba PO2: COPCO FC 3-0 Kajuna FC
Kocha wa Klabu ya Kajuna, Habibu Kondo ameadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kupinga maamuzi ya waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu hadi kutolewa nje kwa kadi nyekundu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:2(2.1) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Mechi Namba PO3: Cargo FC 3-2 Tunduru Korosho
Klabu ya Cargo ya mkoani Dar es Salaam imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la mashabiki wake kufanya vurugu na kutaka kuwashambulia waamuzi wa mchezo huo mara baada ya filimbi ya mwisho.Licha ya kuzuiwa, mashabiki hao walikwenda kuzingira chumba cha waamuzi hadi pale walipoondolewa na walinzi wa uwanjani (stewards).Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 48:1 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba PO4: Tunduru Korosho 1-0 Cargo FC
Wachezaji wa klabu ya Cargo, Bakari Zuberi na Mustafa Hamza wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja kwa kosa la kumpiga mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu mara baada ya mchezo huo kumalizika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:6 (6.3) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mechi Namba PO5: Moro Kids FC 2-3 Tanesco FC
Klabu ya Moro Kids ya mkoani Morogoro imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la mashabiki wake kufanya vurugu na kutaka kuwashambulia waamuzi wa mchezo huo wakiwa wanaelekea kwenye chumba cha kuvalia mara baada ya mchezo kumalizika.Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 48:1 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba PO6: Tanesco 1-2 Moro Kids FC
Mchezaji wa klabu ya Moro Kids, Omari Bakari amefungiwa michezo sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumpiga usoni mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwa kutumia kitu kizito mara baada ya mchezo huo kumalizika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:6(6.3) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Kocha wa makipa wa klabu ya Moro Kids, Agathony Mahenge amefungiwa michezo sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kutishia kumpiga na kumtolea lugha ya matusi mratibu wa mchezo tajwa hapo juu wakati wa mchezo na mara baada ya mchezo huo kumalizika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:2(2.1) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Mtunza vifaa wa klabu ya Moro Kids, Ronal Makoba amefungiwa michezo sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwatolea lugha ya matusi na kuwapiga kwa kutumia chupa ya maji waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakati wakitoka kiwanjani baada ya mchezo huo kumalizika.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 46:2(2.1) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Mechi Namba PO7: Rhino Rangers 5-0 Nyumbu FC
Mchezaji wa klabu ya Nyumbu, Wilfred Amos amefungiwa michezo sita (6) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumpiga usoni mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwa kutumia mpira, mara baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:6(6.3) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mechi Namba PO9: Tanesco FC 3-0 Green Warriors FC
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewaondoa kwenye ratiba ya michezo ya Ligi na kupeleka shauri lao kwenye Kamati ya Maadili ya TFF, waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu ambao ni mwamuzi wa kati Julius William (Manyara), mwamuzi msaidizi namba moja, Jumanne Njige (Mwanza), mwamuzi msaidizi namba mbili, Bernard Tumwine (Kigoma) na mwamuzi wa akiba, Benedict Haule (Morogoro).
Licha ya kufanya maamuzi kadhaa ya utata yaliyoonesha wazi kushindwa kwao kutafsiri sheria 17 za mpira wa miguu katika mchezo huo, waamuzi hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo, jambo ambalo likithibitika watachukuliwa hatua zaidi za kikanuni pamoja na watu wengine wote waliohusika.
Mechi Namba PO10: Green Warriors FC 2-0 Tanesco FC
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewaondoa kwenye ratiba ya michezo ya Ligi na kupeleka shauri lao kwenye Kamati ya Maadili ya TFF, waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu ambao ni mwamuzi wa kati Hamad Augustino (Mara), mwamuzi msaidizi namba moja, Mussa Hemed (Kigoma), mwamuzi msaidizi namba mbili, Baraka William (Dodoma) na mwamuzi wa akiba, Bakari Terema (Pwani).
Waamuzi hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na upangaji matokeo, jambo ambalo likithibitika watachukuliwa hatua zaidi za kikanuni pamoja na watu wengine wote waliohusika.