MSHAMBULIAJI wa Tabora United Offen Chikola amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Azam Rachid Taoussi akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.
Chikola amewashinda Yacouba Sogne wa Tabora United na Moussa Camara wa Simba alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 3 katika dakika 351 alizocheza ndani ya mwezi huo.
Tabora ilizifunga Yanga mabao 1-3, Mashujaa 1-0, KMC 0-2, na ilitoka sare ya mabao 2-2 na Singida Black Stars hivyo kukusanya pointi 10.
Aidha Kocha wa Azam Rachid Taoussi amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Davis Fadlu wa Simba na Hamad Ali wa JKT Tanzania baada ya kushinda michezo mitatu ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo.
Azam walishinda dhidi ya Singida Black Stars 2-1, Yanga 0-1,na Kagera Sugar 1-0 hivyo kupanda hadi nafasi ya 2.
Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa Uwanja wa Lake Tanganyika Shaaban Rajabu kuwa Meneja bora kutokana na usimamizi mzuri wa matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.
Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC kamati imemchagua mchezaji wa Mtibwa Sugar Anuary Jabir kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao manne katika dakika 136 alizocheza akiwashinda Abdulaziz Shahame wa TMA na Naku Kazimoto wa Mbuni.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi novemba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo minne na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya pili mpaka ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo.