GOLIKIPA wa Yanga na Simba, Djigui Diarra na Moussa Camara wameendelea kuwa vinara wa Ligi Kuu ya NBC kwa kuwa na clean sheet 6 kila mmoja hivyo kuzifanya timu hizo kuwa imara eneo la ulinzi.
Diarra wa Yanga amepata Clean Sheet katika mechi 6 za Ligi Kuu ya NBC ambazo hajaruhusu bao lolote hivyo kuifanya kuwa timu pekee ambayo haijafungwa bao katika Ligi Kuu ya NBC.
Kwa upande wa Camara ambaye amecheza michezo 8 ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara 3 katika michezo miwili dhidi ya Coastal Union mabao mawili na mchezo dhidi ya Yanga aliporuhusu bao moja.
Patrick Munthari wa Mashujaa na Metacha Mnata wa Singida Black Star wameshika nafasi ya pili wakiwa na Clean Sheet 5 kila mmoja.
Munthari ameruhusu mabao matatu sambamba na Mnata akiwa ameruhusu mabao matatu.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Zubeir Masoud wa Azam, Musa Mbisa wa Prisons na Ngaleka Katembu wa Dodoma Jiji wakiwa na clean sheet nne kila mmoja.
Nafasi ya nne inashikiliwa na Mohamed Mustapha wa Azam, Denis Donis wa JKT Tanzania, Fabien Mutombola wa KMC na Yona Amos wa Pamba Jiji wakiwa na michezo mitatu bila kuruhusu bao kila mmoja.