LIGI Kuu ya NBC imeendelea katika viwanja vya CCM Liti mkoani Singida na KMC Complex mkoani Dar es Salaam kwa michezo iliyochezwa saa 8:00 mchana na saa 10:00 alasiri.
Ilichukua dakika nane pekee kwa mshambuliaji wa Singida Black Stars Elvis Rupia kufungua ubao wa mabao kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 15 hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 58 Dodoma Jiji walifanikiwa kupata bao kupitia mchezaji wao Yassin Mgaza na kufanya ubao wa mabao kusomeka 2-1 mpaka mwisho wa mchezo huo.
Elvis Rupia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha na kuisaidia timu yake kupata ushindi.
Mchezo wa pili KMC iliikaribisha Mashujaa huku timu zote zikishambuliana kwa kasi hata hivyo ulimalizika kwa suluhu na mchezaji wa Mashujaa Kalos Protas alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.