MZUNGUKO wa nane wa Ligi Kuu ya NBC unazidi kushika kasi ambapo ijumaa michezo miwili ilichezwa mikoa ya Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid na Geita uwanja wa Bukombe.
Mchezo wa Arusha ulianza kwa kasi ikiwa timu za Fountai waliokuwa wenyeji wa Pamba Jiji kutaka alama ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, dakika sita zilitosha kwa timu ya Pamba Jiji kufungua ukurasa wa mabao kupita mchezaji wao Abdallah Ali na dakika sita baadae Fountain Gate walijibu mapigo kupitia mchezaji wao Sadick Ramadhani hivyo mpaka mapumziko ubao ulikuwa 1-1.
Kipindi cha pili kilirejea kwa timu zote kupambana kupata ushindi ambapo hata hivyo juhudi zao hazikuzaa matunda hivyo mchezo ulitamatika kwa sare ya 1-1 na mchezaji wa Fountain Gate Sadick Ramadhani alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Mchezo wa pili ulikuwa katika uwanja wa Bukombe mkoani Geita ambapo timu ya Geita Gold ilikuwa mwenyeji wa timu ya Dodoma Jiji na kupoteza kwa mabao 0-3.
Dakika tatu zilimtosha Khleffin Salum wa Dodoma Jiji kufungua ukurasa wa mabao na dakika ya sita Mwana Kibuta aliiongezea timu hiyo bao la pili na Dodoma Jiji kwenda mapumziko ubao ulikuwa 0-2.
Kipindi cha pili kilirudi Geita Gold wakipambana kuhakikisha walau wanapata chochote lakini juhudi zao hazikuzaa dafu kwani Khleffin Hamdoun alipigilia msumari mwingine kwa Dodoma na dakika 90 kutamatika matokeo yakiwa 0-3.
Khleffin Salum alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha uwanjani ambapo alama tatu ziliiwezesha timu yake kutoka nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC hadi nafasi ya nne.