HAWA HAPA WASHINDI WA TUZO ZA NBC DESEMBA.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Yanga Sead Ramovic akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Mzize amewashinda Prince Dube wa Yanga na Feisal Salum wa Azam alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 4 na kutoa pasi za mwisho 3 katika dakika 288 alizocheza ndani ya mwezi huo.

Yanga ilizifunga Tanzania Prisons mabao 4-0, Dodoma Jiji 0-4 Mashujaa 3-2, na Fountain Gate mabao 5-0 hivyo kukusanya alama 12.

Aidha Kocha wa Yanga Sead Ramovic amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Davis Fadlu wa Simba na Rachid Taoussi wa Azam baada ya kuiongoza Yanga kushinda michezo minne ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar es Salaam, Ashraf Omar kuwa Meneja bora wa uwanja mwezi desemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.

Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC kamati imemchagua mchezaji wa Mbeya City, Kilaza Mazoea kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo kwa mwezi desemba baada ya kufunga mabao manne katika dakika 234 alizocheza akiwashinda Elias Maguri wa Geita Gold/Biashara na Emmanuel Maziku wa Stand United.

Kocha wa Mbeya City Salum Mayanga, amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi desemba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo 3 na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo akiwashinda Awadh Juma wa Mtibwa na Maka Mwalwisi wa TMA alioingia nao fainali.

Mbeya City walizifunga timu za Polisi Tanzania 4-0,Geita Gold 1-0 na Cosmopolitan 1-0.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *