TIMU za JKT Tanzania ya Dar es Salaam, Kitayosce ya Tabora na Mashujaa ya Kigoma zimefanikiwa kupanda Ligi Kuu Ya NBC msimu wa 2023/24 huku kila mmoja akiwa na rekodi zake mpaka kufikia hatua hiyo.
JKT ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu baada ya kushinda michezo mingi zaidi (20) ikikusanya alama 63 na kuizidi timu ya Kitayosce iliyomaliza nafasi ya pili kwa alama tatu.
JKT Tanzania ilikuwa kinara wa kufunga mabao katika Ligi ya Championship ikifunga 48 na kuwa timu pekee iliyofungwa mabao machache (19).
Kitayosce ya Tabora imefanikiwa kupanda Ligi Kuu ya NBC ikiwa imepoteza michezo michache kuliko timu nyingine (4).
Timu hiyo ilipanda daraja baada ya kushinda michezo 18 na kukusanya alama 60 ikiizidi timu ya Pamba iliyokua nafasi ya tatu kwa alama moja.
Kitayosce ilikua timu pekee ya Ligi ya Championship kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni (12) zaidi ya baadhi ya timu zilizoshiriki Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Mashujaa ya Kigoma imefanikiwa kupanda Ligi Kuu baada ya kushinda michezo yake miwili ya hatua ya mtoano dhidi ya Pamba ya Mwanza na Mbeya City ya Mbeya katika matokeo ya jumla.
Mashujaa iliifunga Pamba kwa jumla ya mabao 5-4 na Mbeya City kwa jumla ya mabao 4-2 katika michezo iliyocheza ikiwa uwanja wa nyumbani na ugenini.