TIMU ya Mashujaa ya Kigoma iliyopanda Ligi Kuu ya NBC ikitokea Ligi ya championship imeanza kibabe baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mashujaa ilipata mabao yake kupitia kwa Adam Adam dakika ya 15 na Othman Dunia dakika ya 73 kwa mashuti yaliyopigwa kwa mguu wa kushoto.
Timu ya Kagera imepoteza mchezo wa kwanza wa ligi kwa misimu miwili mfululizo baada ya kupoteza pia kwa Azam ya Dar msimu uliopita kwa mabao 2-1.
Mchezo wa pili siku ya leo haukuweza kuendelea na kumalizwa dakika ya 18 baada ya wachezaji wawili wa Kitayosce kuumia na kusalia sita pekee ambao kikanuni hawaruhusiwi kuendelea na mchezo.
Hadi mchezo huo unamalizwa Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Prince Dube na Feisal Salum ‘Feitoto’ aliyefunga mabao matatu ‘Hat-trick’.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mtibwa Sugar na Simba utakaochezwa uwanja wa Manungu, Morogoro.