PAZIA LA LIGI KUU YA NBC LAFUNGULIWA

Baada ya siku 76 kupita Ligi Kuu ya NBC imerejea tena kwa michezo mitatu iliyochezwa viwanja vya mikoa mitatu tofauti na kushuhudia mabao matano yakifungwa kwa ujumla.

Elias Maguli amekuwa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika msimu huu wa 2023/24 na kuifanya timu ya Geita Gold kupata ushindi wa bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya Ihefu kwenye uwanja wa Highland Estates, Mbeya.

JKT Tanzania mabingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita wameanza vyema ugenini kwa kupata alama tatu dhidi ya Namungo kwa ushindi wa bao moja lililofungwa na Martin Kigi kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Dodoma Jiji imefanikiwa kuwa timu pekee iliyopata ushindi leo ikiwa nyumbani baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union yaliyofungwa na Raizin Hafidh na Meshack Abraham huku Haji Ugando akiifungia Coastal .

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili kati ya Mashujaa iliyopanda daraja na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na Azam itakuwa mwenyeji wa Kitayosce iliyopanda daraja kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *