MZUNGUKO wa 16 umekamilika kwa timu zote za Ligi Kuu ya NBC huku vita ya kuwania ufungaji bora ikizidi kushika kasi na Elvis Rupia akiendelea kushikilia usukani wa kinyang’anyiro hicho.
Rupia anaongoza baada ya kupachika mabao nane hadi sasa na kuisaidia timu yake kufikisha alama 30 na kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Clement Mzize wa Yanga, Jean Ahoua na Leonel Ateba wa Simba wanafuatia wakiwa na mabao saba kila mmoja huku Ateba akifunga penati nne na Ahoua akifunga tatu.
Selemani Mwalimu aliyekuwa Fountain Gate na kusajiliwa na ‘Miamba’ ya soka nchini Morocco Wydad Casablanca amefunga mabao sita sawa na Pacome Zouzoua wa Yanga.
Prince Dube wa Yanga, Edger William wa Fountain Gate na Peter Lwasa wa Kagera Sugar wanafunga msimamo huo wa vinara wa mabao wakiwa na mabao matano kila mmoja.