MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Steven Mukwala amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/25, huku Fadlu Davids pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Mukwala alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Elie Mpanzu wa Simba na Paschal Msindo wa Azam alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ambayo Simba ilicheza mwezi huo na kufunga mabao manne, huku matatu akifunga katika mchezo mmoja (hat-trick). Mukwala alicheza dakika 152 za michezo miwili.
Kwa upande wa kocha Davids aliyeingia fainali na Rachid Taoussi wa Azam na David Ouma wa Singida Black Stars, aliiongoza Simba kushinda michezo yote miwili iliyocheza mwezi huo. Simba iliifunga Dodoma Jiji mabao 6-0 na Coastal Union mabao 0-3, hivyo kuendelea kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Modestus Mwaluka kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Machi kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Wakati huo huo Kamati ya Tuzo za TFF, imemchagua Mwani Thobias wa Mbeya City kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Machi wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Awadh Juma wa Mtibwa Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Thobias aliyeingia fainali na Magata Charles wa Mtibwa Sugar na Selemani Richard wa Stand United, alionesha kiwango chenye mwendelezo, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matano kwa dakika 325 alizocheza za michezo minne.
Kwa upande wa Awadh aliyeingia fainali na Mohamed Ismail wa TMA na Juma Hussein wa Stand United, aliiongoza Mtibwa Sugar kushinda michezo mitatu kati ya minne iliyocheza na kuendelea kubaki kileleni kwenye msimamo wa ligi