LIGI KUU ya NBC inarejea Leo Novemba 8 kwa michezo miwili kupigwa kwenye mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam baada ya kusimama kwa muda kwasababu ya changamoto za kiuendeshaji zilizotokana na sababu za kiusalama na Miongozo yake.
Mkoani Mwanza Pamba Jiji itaialika Singida Black Stars saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Pamba inashika nafasi ya pili (2) kwenye Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikijikusanyia alama 8 kwenye michezo mitano huku Singida BS ikiwa nafasi ya nane (8) na alama zake sita baada ya michezo miwili.
‘Wazee wa kichapo cha Kizalendo’ JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa Mej. Jen Isamuhyo saa 1:00 Usiku. Huu ni mchezo wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC kuchezwa usiku katika uwanja huo.
JKT Tanzania inaingia kwenye mchezo huu ikiwa imefunga mabao Saba na kuruhusu mabao sita kwenye michezo yake mitano iliyocheza, sawa na kusema imefunga na kuruhusu bao katika kila mchezo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2025/2026 huku Simba ikifunga mabao sita na kutoruhusu bao lolote kwenye michezo miwili iliyocheza.
Alama tatu kwa kila timu kwenye michezo ya Leo zinaweza ipa timu yoyote nafasi ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.