WAKALI wa kutumia mguu wa kulia katika kufunga mabao ndani ya Ligi Kuu ya NBC wanazidi kuongezeka kadri Ligi inavyozidi kuendelea ikiwa ni mzunguko wa sita wa Ligi .
Maxi Nzengeli mchezaji anaecheza eneo la kiungo katika timu ya Young Africans amefanikiwa kuifungia mabao mawili timu yake akitumia ufundi wa mguu wake wa kulia na kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani.
Peter Lwasa kiungo mshambuliaji anaekipiga kwenye timu ya Pamba Jiji nae amekuwa hodari na mguu wake wa kulia kwa kuifungia mabao mawili timu yake ndani ya msimu huu.
Mshambuliaji wa timu Mashujaa Mundhir Vuai aliyeanza msimu kwa kiwango bora ameingia pia kwenye orodha hiyo akiwa ameshatupia mabao mawili kwa ufundi wa mguu wake wa kulia.
Coastal Union nao wanatamba na mshambuliaji wao Athuman Makambo ambaye aliwika akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Vijana akiwa na Mtibwa Sugar amefanikiwa kufunga mabao mawili kwa ‘guu’ lake wa kulia.
‘Kino Boys’ timu ya KMC inawakilishwa na Darueshi Saliboko ambaye amefunga mabao mawili kwa mguu wake wa kulia huku moja ya bao hilo likiwa bao la kwanza la msimu wa 2025/2026.
Mkongwe Vitalis Mayanga wa timu ya Mbeya City anazidi kuwafundisha vijana kuwa mguu wake wa kulia bado upo vizuri akifanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya msimu huu.
Andy Boyeli ambaye jina lake halikuimbwa sana wakati wa usajili wake ni mshambuliaji wa timu ya Young Africans ambaye hadi sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani mara mbili kwa mguu wake wa kulia akifunga yote kwenye mchezo dhidi ya KMC.