TAYARI michezo 176 kati ya 240 ya Ligi ya Championship ya NBC imeshachezwa huku ushindani mkubwa ukionekana baina ya timu zinazoshiriki ligi hiyo ambayo Mtibwa Sugar ipo kileleni kwasasa ikiwa na alama zake 54 baada ya michezo 22 ya Ligi hiyo.
Kwa upande wa nafasi nne za juu ushindani ni mkubwa huku kila timu zikitafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC moja kwa moja ambapo nafasi hizo nne za juu zinashikiliwa na Mtibwa akiwa nafasi ya kwanza na alama 54, Mbeya City ikiwa nafasi ya pili ikiwa na alama 46 sawa na Stand United iliyo nafasi ya tatu wakitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa na nafasi ya nne ikishikiliwa na Geita Gold yenye alama 45.
Cosmopolitan, African Sports, Transit Camp na Biashara United zinaendelea kupambana kwenye nafasi nne za chini kujinasua kutokushuka daraja kwa msimu huu, Biashara United inaburuza mkia kwenye Ligi hiyo ikiwa na alama nne pekee, Transit Camp ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 11, African Sports inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 14 wakati Cosmopolitan ikiwa na alama 15 kwenye nafasi ya 13.
Timu mbili za juu kwenye msimamo zinapanda moja kwa moja kwenye Ligi Kuu ya NBC huku mbili za mwisho zikishuka moja kwa moja na kushiriki First League.