LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo miwili ambapo Pamba Jiji iliwakaribisha timu ya Azam katika mchezo uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Namungo iliwakaribisha Dodoma Jiji uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Mchezo wa Pamba Jiji ulianza majira ya saa kumi alasiri ambapo timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa kasi na kuonyesha nia ya kuzitaka alama zote tatu mhimu za mchezo huo hivyo kwenda mapumziko wakiwa suluhu ya kutokufungana bao lolote.
Kipindi cha pili kilianza ambapo Pamba Jiji ilionekana kurejea kwa kasi zaidi huku ikizima mashambulizi yaliyokuwa wakianzishwa na Azam mara kwa mara na dakika ya 86 ya mchezo huo Pamba Jiji walipata bao kupitia mchezaji wao Deus Kaseke ambae aliingia dakika chache kabla ya kufunga bao hilo pekee lililopeleka kilio kwa ‘matajiri wa jiji la Dar es Salaam’ baada ya mchezo kuisha kwa Pamba 1-0.
Mchezo wa pili ulianza majira ya saa moja jioni ambapo Namungo ‘Wauaji wa Kusini’ iliwakaribisha Dodoma Jiji huku timu ya Namungo ikionekana kushambulia zaidi.
Iliwachukua dakika 21 timu ya Dodoma Jiji kupitia mchezaji wao Paul Peter kufungua ukurasa wa mabao na dakika kumi mbele Apolo Otieno aliiongezea bao la pili Dodoma Jiji na dakika ya 44 Namungo walipata bao kupitia mchezaji wao Pius Buswita hivyo kwenda mapumziko ubao ukisoma 1-2.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Namungo wakisaka bao la kusawazisha huku Dodoma Jiji wakisaka bao zaidi, dakika ya 56 ya mchezo huo mchezaji wa Namungo Erasto Nyoni aliiongezea timu yake bao la pili kupitia mkwaju wa penati hivyo matokeo kuwa 2-2 mpaka mwisho wa mchezo.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo katika viwanja vitatu ambapo KenGold watawakaribisha Fountain Gate katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na mkoani Dar es Salaam KMC watawakaribisha Singida Black Stars huku JKT wakiwakaribisha Young Africans uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.