Ligi Kuu ya NBC msimu wa wa 2026/27 iliendelea kutimua ‘vumbi’ kwa timu za Simba, TRA United na Mashujaa baada ya kushinda michezo yao wakiwa uwanja wa nyumbani.
Katika mchezo wa mapema uliochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid TRA United ilibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Fountain Gate.
TRA united ilipata mabao yake kupitia kwa Anni Elijah dakika ya 31, emmanuel Mwanengo dakika ya 38 na Amy Mapaka dakika ya 89 aliyehitimisha mabao ya TRA United.
Kwa upande wa Fountain Gate mabao yalifungwa na Hashimu Kindemile dakika ya 60 na Chukwunonye Obasi dakika ya 65 akiwapa Fountain mabao ya kufutia machozi.
Nayo Mashujaa ilitumia vyema uwanja wa nyumbani wa lake Tanganyika mkoani Kigoma baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji.
Crispin Ngushi ndiye aliyeiweka Mashujaa mbele kwa kufunga bao la pekee la mchezo dakika ya 20 lililodumu hadi filimbi ya mwisho na kuipa alama zote tatu huku Pamba jiji wakipoteza alama wakiwa ugenini.
Katika mchezo uliochezwa uwanja wa uhuru jijini Dar es saalam timu ya Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo katika pambano lililokuwa na ushindani mkubwa huku Simba ikiendelea kusalia kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Simba ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya nne kupitia Anicet Oura lakini Namungo ilisawazisha dakika ya 35 kupitia Raymond Lulendi kabla ya mshambuliaji huyo kuongeza bao la pili dakika ya 43 na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili Simba ilirejea na kusawazisha dakika ya 79 kupitia Rushine De Reuck kwa mkwaju wa Penati na Anicet Oura kuhitimisha bao la tatu dakika ya 88 na kufanya Simba kuendeleza rekodi ya ushindi wa asilimia 100.