LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa mchezo mmoja uliochezwa katika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam Simba waliwakaribisha KMC majira ya saa 10 alasiri na kufanikiwa kushinda 4-0.
Awesu Awesu alifungua ukurasa wa mabao dakika 25 ya mchezo huo baada ya kupokea mpira kutoka kwa mshambuliaji wa timu hiyo Steven Mukwala hivyo kuiweka mbele timu yake ya Simba.
Dakika ya 38 ya mchezo Jean Ahoua alifanikiwa kuipatia timu yake bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa KMC, Raheem Shomari kufanya faulo kwa Shomari Kapombe hivyo Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
Baada ya mapumziko mchezo uliendelea kwa timu zote mbili kushambuliana kwa kasi na dakika ya 66 Edwin Balua alifanikiwa kuiongezea timu yake bao la tatu akipokea pasi kutoka kwa Valentin Nouma huku bao la mwisho likifungwa na Jean Ahoua dakika ya 69 ya mchezo huo na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Ligi Kuu ya NBC itaendelea katika Uwanja wa Azam Complex ambapo Yanga watawakaribisha timu ya Tabora United mchezo utakaochezwa saa 12 jioni.